Dar es Salaam. Sikukuu ya Krismasi kwa mwaka huu huenda ikakumbukwa kwa mambo mengi kulingana na jinsi mtu alivyojipanga kuisherehekea.
Yapo mambo mazuri yaliyofanyika, lakini yapo pia kero zilizotokana na sikukuu hiyo.
Katika misa mbalimbali zilizofanyika, viongozi wa dini walihimiza mambo manne katika mahubiri yao ambayo ni amani, kusameheana na viongozi wa Serikali kuombewa ili watende haki huku wakionya kuhusu utoaji wa mimba na talaka.
Miongoni mwa kero na mambo mabaya yaliyojitokeza ni pamoja na ajali zilizotokana na ulevi, migogoro ya ndoa na mahusiano, kuongezeka kwa maambukizi ya maradhi ya zinaa na madhara ya kiafya.
Utafiti uliofanywa na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Washington nchini Marekani umebaini kuwa ndoa nyingi huvunjika baada ya sikukuu za mwisho wa mwaka.
Wasomi hao ambao ni Profesa Julie Brines na Brian Serafini wanasema shinikizo la sherehe za Krismasi mara nyingi huathiri ndoa iwapo mambo yaliyopangwa na familia yakishindwa kutimizwa.
“Lakini ndoa zenye matatizo zenyewe hudhani kuwa sikukuu ni wakati mzuri wa kuimarisha uhusiano na kuanza upya. Wanafikiri kuwa na Krismasi yenye furaha pamoja na familia zao au kuwapeleka watoto safari. Watu wanakuwa na matarajio mengi licha ya changamoto walizokuwa nazo siku za nyuma,” anasema Profesa Brines.
Wanaeleza kuwa endapo matarajio hayo yasipotimia, huongeza mivutano ya kifamilia na kuvunjika moyo kwa wanandoa, jambo linalosababisha baadhi yao kutengana kabisa.
Pia, wanasema masuala ya kifedha wakati wa Krismasi huchangia hali hiyo kutokana na mazoea ya wengi kutumia fedha kiholela na baada ya sherehe kumalizika hukumbana na hali ya ukata inayosababisha migogoro ya kifamilia.
“Hii inatokana na kuwa baada ya sherehe za mwisho wa mwaka, mahitaji ya fedha huongezeka kwa sababu ni msimu wa kupeleka watoto shule, kulipa kodi za nyumba na mambo mengi yanayohitaji fedha,” anasema Profesa Serafini.
Anasema tabia ya watu wengi kuamua kusherehekea sikukuu hizo kwa gharama za kupindukia hususan katika vilevi, imetajwa kuwa kishawishi cha wengi kushiriki ngono ovyo suala ambalo ni tishio kwa ndoa na mahusiano ya wapenzi ambao bado hawajafunga ndoa.
Mtaaalamu wa saikolojia, Charles Nduku anasema kwa hapa nchini mambo hayo hutokea kutokana na watu kuwa na furaha kupindukia baada ya kusubiri kwa muda mrefu.
Anasema hali hiyo husababisha watu kutumia hata akiba ya fedha kwa ajili tu ya sherehe, jambo ambalo huwafanya kuathirika kiuchumi baada ya sherehe.
“Mara nyingine ni kukosa self-control (kujidhibiti) kwa mtu binafsi kwa sababu kuna maisha hata baada ya sikukuu. Ikifika sikukuu watu wanalewa, wanachepuka kiholela na mara nyingine ni kama kuiga kwa sababu kila mtu anafanya hivyo,” alisema Nduku.
Kabla ya Krismas, Jeshi la Polisi lilitahadharisha juu ya ajali zinazoweza kutokea kutokana na ulevi, hivyo liliwataka madereva wa vyombo vya moto kuepuka matumizi ya pombe ili kuepuka ajali.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Ahmed Msangi alipozungumza na Mwananchi juzi, alisema katika sikukuu hiyo hakukuwa na matukio mengi ya kutisha isipokuwa yale ya kawaida.
Alitoa tahadhari kwa wananchi kuendelea kusherehekea sikukuu zijazo kwa amani huku akisema suala la usalama ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
“Sijaona ripoti yoyote mbaya ya ajali kubwa, lakini kwa ujumla ni matukio yale ya kawaida ambayo yanatokea hata siku za kawaida,” alisema Msangi.