Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo ameagiza Wizara za fedha na ya Kilimo kushirikiana ili walipe fedha za wakandarasi wanaojenga miradi mikubwa ya kimkakati.
Chongolo ametoa agizo hilo leo Jumapili Juni 18, 2023 wakati akizungumza na wanaushirika wa Kilimo cha zabibu katika shamba la Chinangali Chamwino. Katibu Mkuu amesema katika ziara zake amebaini kuwa baadhi ya miradi wakandarasi hawalipwi kwa kadri mikataba inavyosema.
Ametoa agizo hilo leo wakati akikagua mradi wa umwagiliaji wa shamba la zabibu la ushirika Chinangali. Chongolo amesema baadhi ya miradi amebaini fedha zake hazitoki kama inavyotakiwa lakini sababu hazijulikani.
"Nimeongea na Waziri wa Fedha leo (Dk Mwigulu Nchemba) lakini majibu yake ni kuwa tunatekeleza, sasa nataka mkutane watu wa Kilimo na Fedha, mtuambie mkakati wa kulipa wakandarasi," amesema Chongolo.
Amezungumzia mradi wa bwawa la umwagiliaji la Msagali Mpwapwa kwamba mkandarasi wake hajalipwa fedha kama inavyotakiwa.
Chongolo amesema kitendo hicho kinapoteza muda wa umaliziaji wa mradi kulingana na mkataba unavyosema.
Mbali na mradi wa bwawa la umwagiliaji la Msagali, amesema mradi wa Kilimo cha zabibu Chinangali nao unahitaji msukumo wa fedha.