Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo aibana Duwasa kero ya maji kibaigwa

Duwasa Picd Chongolo aibana Duwasa kero ya maji kibaigwa

Sun, 18 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), wameeleza mkakati wa kuimarisha huduma za maji katika mji mdogo wa Kibaigwa ambako kumekuwa na kero ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu.

Mkurugenzi wa Duwasa, Aron Joseph amesema mkakati wa kupeleka maji katika mji huo katika hatua ya kwanza itakuwa ni kuchimba visima ili kukabiliana upungufu wa maji.

Aron ametoa maelezo hayo jana jioni Jumamosi Juni 17, 2023 baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kumtaka ajibu mbele ya wananchi namna ya kuondokana na kero ya upungufu wa maji kwenye mji huo unaokua kwa kasi.

Kibaigwa ni eneo linaloshika nafasi ya pili kwa wingi wa watu kati ya Kata 209 zinazounda mkoa wa Dodoma ikiwa nyuma ya Kata ya Nzuguni lakini maeneo hayo yanakabiliwa na kero ya maji.

Mkurugenzi alisema Duwasa imekabidhwa kuhudumia mji huo rasmi Juni 9, 2023  na imeanza kutoa maji kwa mgao kutokana na uzalishaji kuwa mdogo ikilinganishwa na mahitaji.

Kwa mujibu wa Aron, mahitaji ya maji katika mji huo ni lita 3.7 milioni kwa siku na uwezo wa kuzalisha ni lita 2.3 milioni na hivyo kuwa na upungufu wa lita milioni 1.4 kwa siku.

“Hata hizo lita 2.3 milioni hatuzizalishi inavyotakiwa kutokana na changamoto ya umeme na tumekuwa tukizalisha kwa saa 10 hadi saa 12, hivyo wananchi hawa wanaweza kupata maji mara mbili ya wanavyopata sasa kama tutakuwa na umeme wa uhakika.”amesema Aron.

Aidha, Aron amemuomba Chongolo amsaidie kumuombea kwa wananchi waridhie kutoa maeneo yao ili Duwasa ianze kuchimba visima vya maji hata kabla ya ulipaji wa fidia kwani mahitaji ya maji ni makubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live