Wananchi wanaozungukwa na miradi ya maendeleo wametakiwa kukataa fidia za fedha badala yake wapewe Ardhi mbadala.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi Juni 17, 2023 na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo alipotembelea mradi wa bwawa la maji la Msagali wilayani Mpwapwa.
Chongolo amesema maeneo mengi wananchi wanapopelekewa miradi mikubwa ya maendeleo wamekuwa wakilipwa fidia na kutakiwa kupisha jambo ambalo si sahihi.
Amesema mpango wa kuwalipa fidia wananchi kwenye miradi ya maendeleo halafu wanaambiwa waondoke ni kupishana na fursa.
"Msikubali hata kidogo kuondoka karibu na maeneo haya, wambieni wawape fidia ya ardhi mbadala ili mbaki karibu na miradi ambapo mtakuwa wanufaika, kataeni kupokea fedha kwenye ardhi yenu," amesema Chongolo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, miradi inapelekwa kwa ajili ya watu lakini inapotokea wahusika wa maeneo ya mradi kuondoka si jambo la heri hata kidogo.
Akizungumza kuhusu Ujenzi wa miradi, alisisitiza kukamilika kwa wakati kama ambavyo mikataba imeelekeza.
Mradi wa umwagiliaji katika bwawa la Msagali unajengwa kwa gharama ya Sh27.8 bilioni ukilenga wanufaika katika vijiji vya Msagali, Chunyu, Nghambi na vitongoji vya vijiji vya Igandu.