Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo: Ajenda ya lishe iwe ya kudumu Songwe

Chongolo Weeeeb Mkuu wa mkoa wa Songwe Daniel Chongolo

Wed, 12 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Mabaraza ya madiwani mkoani Songwe yametakiwa kubeba ajenda ya lishe kwenye vikao ili kukabiliana na tatizo la udumavu na utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano unaoukabili mkoa huo.

Wito huo umetolewa leo Juni 12 na mkuu wa mkoa huo Daniel Chongolo kutokana na takwimu kuonyesha kuwa asilimia 31.9 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wana udumavu na utapiamlo licha ya kuwa miongoni mwa mikoa mitano inayozalisha chakula kwa wingi nchini.

Chongolo amesema hayo kwenye Baraza la Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Songwe lililokuwa likijadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo amesikitishwa na takwimu za utapiamlo na udumavu.

Hivyo amewataka madiwani wa halmashauri zote mkoani humo kuibeba ajenda ya lishe kwenye vikao vyao, kuona namna bora ya kukabiliana au kuondoa kabisa hali hiyo.

“Aibu mkoa wetu kuutaja kuwa na changamoto ya udumavu na utapiamlo kisa ukosefu wa lishe wakati tunasifika kwa uzaishaji wa aina mbalimbali za vyakula. Hii haikubaliki, kila mmoja awajibike kuondoa changamoto hii,” amesema Chongolo.

Amewataka waganga wakuu wa wilaya kupanga ratiba ya kutoa elimu kwa wananchi ili wajue matumizi ya vyakula wanavyozalisha, waondokane na udumavu na utapiamlo.

“Tumekuwa tukilalamika wanafunzi kufeli bila kuangalia aina ya vyakula wanavyokula ambavyo si mlo kamili na mtoto hawezi kufanya vizuri, hii ajenda iwe ya kudumu,” amesema.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Songwe, Abraham Sambila amesema watahakikisha ajenda ya lishe inakuwa endelevu kuanzia ngazi ya vijiji ili kuondoa aibu ya udumavu unaoshamiri kwa watoto licha ya kuzalisha vyakula vingi.

Mkazi wa Songwe, Asangalwisye Mwashambwa amesema walezi wa kiume wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya lishe bora mara kwa mara ili wawahimize wenza wao kuzingatia hilo ili kuwanusuru watoto walio chini ya miaka mitano kupata udumavu.

Chanzo: Mwananchi