Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chifu akerwa wazazi kupokea mahari za mabinti walio shule

Fri, 12 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chifu wa kabila la Wagogo jijini Dodoma, Lazaro Masuma ameiomba Serikali kukomesha vitendo vya baadhi ya wazazi kupokea mahari ya awali kwa ajili ya kuwaoza mabinti zao wakiwa bado shuleni.

Chifu Masuma ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Oktoba 10, 2018 wakati akichangia mjadala kuhusu changamoto za mimba na ndoa za utotoni ulioingia siku ya pili ambao umeandaliwa na Shirika Kimataifa linaloshughulisha na Idadi ya Watu (UNFPA).

UNFPA imeshirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau mbalimbali kikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yatakayofanyika kesho.

Chifu Masuma amesema vitendo hivyo hujitokeza zaidi wilaya za Bahi na Chamwino kwa wazazi wa kupokea mahari za awali kwa binti zao wanaosoma kuanzia darasa la nne na kuendelea.

“Mipango hii inafanyika kwenye vilabu vya pombe na mahari zinazotolewa ni mifugo hasa ngo’mbe. Mtoto anasoma lakini tayari ameshawekewa oda, ikitokea amemaliza na kufaulu mzazi anamwambia haina haja ya kuendelea na shule kwa sababu nimeshapokea mahari yako,” amesema.

“Ukifika kijijini utaona mzee ana mabinti wengi, unaweza ukadhani ni wajukuu kumbe ni wake zake. Hili jambo la kawaida Dodoma,” anasema Chifu Masuma.

Amesema hana nguvu ya kutosha ya kuchukua hatua dhidi ya tatizo hilo kwa kuwa hajapewa rungu na mamlaka husika lakini Serikali ikiingilia kati changamoto hiyo itakwisha.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jinsia, Dk John Jingu amesema Serikali itafuatilia jambo hilo ili kuhakikisha vitendo hivyo vinadhibitiwa na watoto wanapata haki zao za msingi.

Pia, amewaomba viongozi wa kidini na kimila kushirikiana na Serikali katika jitihada za kukabiliana na vitendo hivyo kwa sababu wao wana nafasi pia.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz