Serikali Mkoa wa Mwanza imeagiza wilaya za mkoa kuhakikisha fedha zilizobaki baada ya kukamilisha miradi ya ujenzi wa maradasa ya Uviko-19 zielekezwe kujenga vyoo vya wanafunzi kwenye shule husika.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Januari Mosi 2022 na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ngussa Samike alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi ya vyumba vya madarasa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Amesema jambo lililofanywa na Serikali kuzielekeza fedha kujenga vyumba vya madarasa kwenye shule za Sekondari linapaswa kuungwa mkono hivyo chenji zilizobaki zikajenge vyoo vya wanafunzi.
Amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ambapo wilaya ya Sengerema inatakiwa kuvikabidhi Januari 5 mwaka huu.
"Sengerema mmefanya kazi vizuri na zinaonekana sasa kazi imebaki kuhamasisha wanafunzi wote kuingia shule zitakapofunguliwa" amesema Samike.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema, Birunu Shekidele amesema watatekeleza maagizo yote waliyopewa na kuhakikisha chenji hizo zinajenga vyoo vya wanafunzi ili kuwaondolea adha ya kupata mahali pa kusaidia.
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ilipokea Sh2.5 bilioni kujenga madarasa 129 kwenye shule za sekondari na kwa sasa yamefika asimilia 98 ambapo wanatarajia kuyakabidhi Januari 5 mwaka huu.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Ngweri, Nelson Rwelengera ameishukuru Serikali kwa kufanikisha mradi huo akisema kwa sasa hakutakuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwenye shule za sekondari.
Diwani wa Kata ya Ibisageni, Jumanne Masunga amesema wananchi wamefurahishwa na mradi huo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa hali inayowapunguzia mzigo wa michango mbalimbali.