Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chemchemi ya maji moto Songwe inavyoanza kutoa fursa

47b526bdaaa51c877d99c952e2a8974b Chemchemi ya maji moto Songwe inavyoanza kutoa fursa

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKOA wa Songwe ni mkoa uliyojaaliwa kuwa na vivutio vingi ambavyo vikiendelezwa ni vyanzo vizuri vya utalii.

Miongoni mwa vivutio hivyo ni chemchemi ya maji ya moto iliyoko Nanyara (Mbozi), mapango ya popo (Mbozi), Kimondo Ndolezi (Mbozi), unyayo wa binadamu wa Kale Nkangamo (Momba) na Bwawa la Chumvi la Itumbula (Momba).

Vingine ni maporomoko ya maji (Ileje), matanuri ya binadamu wa kale (Momba), madini ya marumaru (Mbozi), makaa ya mawe (Mbozi), madini ya chokaa pamoja na Mbuga ya wanyama ya Pit Lukwati iliyopo wilaya ya Songwe.

Katika makala haya, mwandishi anaangazia chemchemi ya majimoto iliopo Nanyala, Mbozi, ambayo imekuwa ikitumiwa na wakazi wa eneo hilo katika shughuli zao za kimila ambayo sasa imegeuka kuwa na fursa nyingi za kiuchumi.

Fursa hizo zinatajwa kuwa ni chemchemi hiyo kutumika kwenye miradi ya ufuaji wa umeme, utalii, kilimo, ufugaji wa kuku na ufugaji samaki.

Fursa hizo zikitumika kama inavyotarajiwa zinatazamiwa kubadilisha maisha ya wananchi wa Kata ya Nanyala, mkoa wa Songwe na Taifa kwa ujumla.

Hatua hii imekuja baada ya serikali kupitia Wizara ya Nishati kuamua kuwekeza katika mradi wa umeme wa jotoardhi (Geothemo) kupitia Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Meneja wa TGDC, Kato Kabaka, anasema baada ya kufanya utafiti wamebaini kuwa Mradi wa Jotoardhi Nanyara unaweza kuzalisha kuanzia megawati tano hadi 38 za umeme hadi kufikia mwaka 2023 zitazochangia upatikanaji wa umeme nchini.

Kabaka anasema umeme wa nishati wa jotoardhi ili uanze kuzalishwa kunahitajika nyuzi joto 100 mpaka 140 lakini joto linalopatikana hivi sasa ni nyuzi joto 70 ambalo linafaa kwa matumizi mengine ya nishati.

"Nyuzi joto 70 tulizozifikia ambazo zinapatikana hivi sasa kwenye chemchemi juu ya sura ya dunia zinatupa fursa ya kutumia joto hili moja kwa moja katika uzalishaji wa miradi mbalimbali na kunufaisha wananchi wa maeneo haya na taifa kwa ujumla pasipo kulibadilisha joto hilo," anasema Mhandisi Kabaka.

Mhandisi huyo anasema shughuli za utafiti wa kina wa nishati ya jotoardhi katika miradi huo mpaka sasa wamefikia hatua ya uchorongaji visima vya jotoardhi ili kuhakiki kiwango cha hifadhi halisi ya joto lililoko chini ya ardhi.

Anafafanua kwamba katika mradi huo wa Nanyala, tayari wamefikia kati ya nyuzi joto 50 mpaka 70 na wanaamini watafikia nyuzi joto 100 kutokana na kuzidi kuchimba kwa kushuka chini.

Miradi ya kuvutia uwekezaji

Kabaka anasema pamoja na tafiti kuonyesha kuwa jotoardhi (chemchemi ya maji moto) ni chanzo kizuri kwa ajili ya nishati ya umeme, wakati wanaendelea na jitihada za uendelezaji wa nishati hiyo ya jotoardhi wamefanikiwa kubuni miradi kupitia teknolojia ambazo zinawawezesha wananchi na wawekezaji kuanza kunufaika na jotoardhi kiuchumi.

Manufaa hayo anasema ni pamoja na kuanzisha mradi wa ufugaji kuku kwa kutotoresha mayai, kuwa na mtambo wa kukausha mazao, mradi wa samaki, mradi wa kilimo cha mbogamboga na mradi wa bwawa la kuogelea.

"Wakati tunaanaendelea na mchakato wa kukamilisha uzalishaji wa umeme watalaamu wetu kutoka TGDC wamebuni teknolojia ya utotoleshaji wa vifaranga kwa kutumia nishati ya jotoardhi kwa kutumia kifaa cha kudhibiti joto la maji moto," anasema Kabaka.

Anasema wameanza pia kutengeneza sehemu za kuogelea ambapo watalii kutoka ndani na nje watapa fursa ya kuogelea wakati wakipata mapumziko kwa kuwa maji hayo yana joto na madini ambayo yana faida kwenye mwili wa binadamu.

Kuhusu mradi wa samaki anasema jotoardhi linatoa nishati ambayo husaidia samaki kukua kwa haraka.

Kilimo cha mboga mboga, ukaushaji mazao

Mhandisi Kabaka anasema jotoardhi inatoa mazingira ya kuanzisha kilimo cha mboga mboga, maua na matunda.

Anasema joto na ukaa hufanya mazingira kuwa mazuri katika kustawisha mazao hayo kwa maana ya kuzaa zaidi na kukomaa kwa muda mfupi.

"Tunajua mkoa wa Songwe unazalisha kwa wingi mazao kama kahawa, mahindi, mchele na mazao mengine. Mpango wetu ni kutengeneza mtambo wa kukausha mazao kwa kutumia jotoardhi, mtambo huo utasaidia ubora wa mazao kuwa mazuri, utapunguza upotevu wa mazao ambao hutokea kipindi cha kuanua na kuanika na kuondoa shida ya sumu kuvu ambayo hutokea kutokana na mazao kutoanikwa vizuri," anasema Kabaka.

Antony Aloyce, mbunifu wa kifaa cha kibadilisha joto anasema kazi ya kifaa hicho ni kubadilisha joto la maji ya moto na kulifanya liweze kutumika katika kilimo cha mboga mboga na matunda.

Anasema pia teknolojia hiyo inabadilisha joto na maji ya moto ili yaweze kutumika katika kuzalishia samaki pamoja na kubadilisha joto hilo katika ukaushaji wa mazao mbalimbali.

Kutotolesha vifaranga

Anasema kwa kutumia maji moto watalaamu wamebuni na kutengeneza mtambo wa kutumia maji moto kutotoleshea vifaranga kwa wingi, mradi ambapo tayari mazao ya kwanza ya majaribio yapo na kuku wameshakuwa wakubwa.

"Wawekezaji wa ndani wanakaribishwa kuja kuwekeza kwenye ufugaji, sisi tutawapatia nishati na teknolojia ambapo tutakuwa tumechangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza thamani ya mazao ya kuku," anaongeza Kabaka.

Aman Cristopher, mgunduzi wa mashine ya kutotolesha mayai kwa kutumia jotoardhi anasema Tanzania ina mahitaji makubwa ya bidhaa za kuku hususani nyama na mayai ambazo hutumika kama chakula.

“Uzalishaji wa mazao haya nchini ni mdogo hivyo Watanzania wanalazimika kuagiza bidhaa hizo kutoka mataifa ya nje. Hii ni kutokana na uzalishaji kwa njia za kienyeji kwa mtu mmoja mmoja na pia uwepo wa gharama kubwa za kufanya uzalishaji wa kisasa na wa kibiashara," anasema Amani.

Anasema kimsingi Tanzania ina nishati kubwa ya jotoardhi ambayo ina gharama nafuu. Anasema nishati hiyo ikiendelezwa inaweza kutumika kuendesha mashine za kutotoa vifaranga kwa kuvuna tu joto lililoko kwenye majimoto.

"Hilo ndilo lililotupatia msukumo wa kutengeneza teknolojia hii. Wazo ni la TGDC, mimi ni mtaalamu niliyefanya utekelezaji wa kubuni teknolojia hii," anasema Amani.

Waziri wa Nishati, Medard Kalemani akiwa katika ziara ya kutembelea mradi huo wa umeme wa jotoardhi anasema Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati ya jotoardhi na kwamba wizara yake imeanza kuvitembelea ili viweze kufahamika.

Anasema katika mikoa ya Mbeya na Songwe pekee kuna miradi inayoweza kuzalisha zaid ya megawati 165 za joto ardhi na kuna maeneo mengine anayataja kuwa ni Natron (Arusha), Kyejo Mbaka (Mbeya), Luhoi (Pwani) pamoja na Songwe ambako huo uko mbioni kuanza kuzalisha umeme.

Waziri Kalemani anasema kwa ujumla hifadhi ya jotoardhi inayopatikana hapa nchini ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 5,000 za umeme katika miaka kumi ijajayo ikiwa watajipanga vizuri.

Anasema kiasi hicho cha umeme kitasaidia kwa kiasi kikubwa kwenye kuleta maendeleo ya uhakika nchini kutokana na nchi kujielekeza kwenye uchumi wa viwanda unaotegemea upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Anasema kwa sasa Tanzania inazalisha megawati 1602 za umeme lakini bado hakuna megawati hata moja itokanayo na jotoardhi.

"Kwa kuanzia Wizara ya nishati tutaanza na megawati 200 za umeme wa Joto ardhi ambazo zitaanza kupatikana, miongoni mwa hizo ni megawati 5 hadi 38 zitakazozalishwa hapa kwenye mradi wa Jotoardhi Songwe," anasema Dk Kalemani.

Dk Kalemani pia amemtaka Meneja wa Kampuni ya uendelezaji wa Jotoardhi Tanzani (TGDC) kuharakisha utengenezaji wa miundombinu itakayowezesha upatikanaji wa umeme unaotokana na jotoardhi.

Anamtaka pia kutumia miaka miwili kuanza kuzalisha umeme usiopungua megawati 200 ili nchi ianze kunufaika na nishati hiyo ya jotoardhi.

Mkuu wa mkoa wa Songwe, Nicodemas Mwangela anasema kutokana na vitu vingi vya uwekezaji na utalii kupatikana eneo hilo, anamwomba waziri ikiwezekana sehemu hiyo iitwe 'Kituo cha Utalii Songwe' ili kuwavutia watalii zaidi kutoka sehemu mbalimbali.

Anasema eneo hilo la Nanyala pia lina kivutio cha mapango ya popo ambayo yapo umbali wa takribani kilomita 10 kutoka eneo la mradi huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Msyani ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nanyala palipo na mradi wa hotoardhi anasema wakazi wa eneo hilo wao huwa wanatumia maji hayo ya moto katika shughuli mbalimbali za kimila.

Anasema maji hayo hutumika katika matambiko mbalimbali ya kutoa mikosi na pia akina mama wajawazito toka miaka yote hutumia maji hayo wakiamini kuwa huwasaidia kujifungua bila matatizo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Majimoto, Philemon Namwema anaongeza kwamba wamekuwa wakijipatia magadi kwa ajili ya mifugo kutokana na maji hayo kusheheni magadi na kwamba nyasi za eneo hilo hutumika kwa kutengenezea vikapu.

"Kwa upande wa mila wakazi wa hapa hutumia udongo wa hapa majimoto kuwapaka watoto wenye ukurutu mwilini na maji haya pia wenyeji wanayahusisha na kumwondolea mtu mikosi,” anasema Namwema.

Chanzo: habarileo.co.tz