Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chemba kupata mamlaka ya maji

5646604500ce2d0dc7fd39aec441d552 Chemba kupata mamlaka ya maji

Mon, 14 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inapanga kuanzisha Mamlaka ya Maji Chemba.

Ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi Mnadani, Kijiji cha Kelema, Kata ya Paranga, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.

Katika mkutano huo, Majaliwa aliwaombea kura mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Rais John Magufuli, mgombea ubunge Jimbo la Chemba, Mohammed Moni na wagombea udiwani.

"Wilaya hii haina mamlaka ya maji. Tutaanzisha Mamlaka ya Maji ili watumishi wawepo wilayani na wasimamie kwa karibu na waweze kufuatilia vyanzo vya maji kutokea hapa Chemba wakati tukiendelea kutatua tatizo la maji wilayani hapa. Tutaunda mamlaka ya maji hivi karibuni," alisema Majaliwa.

Amesema Serikali ilitoa Sh bilioni 1.688 kutafuta vyanzo vya maji Orada, Kisanga, Moi, Mondo na Ndaki.

"Serikali ya Awamu ya Tano pia imetoa Sh milioni 677 za kuchimba visima huko Mondo, Mrijo Juu, Chambalo, Hamai na Chemba," alisema.

"Tuna uhakika tukipata lita za maji za ujazo 4,700 zinatosha kabisa kujenga mtandao wa maji. Kazi ya kuboresha miundombinu ya maji inaendelea. Zimetengwa fedha nyingine, Sh milioni 150 za kusambaza maji Kelema, Msaada na Bumbu."

Akizungumzia sekta ya afya, Majaliwa alisema zimetolewa Sh bilioni 1.8 kujenga Hospitali ya Wilaya ya Chemba ili wananchi wapate huduma za tiba badala ya kwenda Kondoa.

"Nia yetu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hukohuko aliko kwa kuweka zahanati katika kila kijiji, vituo vya afya kwa kila kata. Wakimaliza ujenzi, tumetenga shilingi milioni 500 za vifaa vya hospitali kwa majengo yote saba," alisema.

Akaongeza: "Tumepeleka Sh milioni 400 za Kituo cha Afya kule Hamai, Sh milioni 500 kule Mrijo na Sh milioni 400 kule Kwa Mtoro. Kazi ya ujenzi ikiisha, kila kimoja kitapata Sh milioni 250 za vifaa vya tiba."

Chanzo: habarileo.co.tz