Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chaula ataka mikopo Simanjiro kurudishwa kwa wakati

60903 Pic+chaula

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Simanjiro. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Zephania Chaula amewataka wanawake, vijana na walemavu waliopatiwa mikopo kupitia makusanyo ya ndani ya Halmashauri hiyo kurudisha kwa wakati.

Chaula ameyasema hayo wakati wa kukabidhi hundi ya mikopo ya Sh230.8 milioni kwa vikundi 59 vya wanawake, vijana na walemavu jana Mei 31 mji mdogo wa Orkesumet.

Amesema vikundi hivyo vilivyopokea mkopo huo warejeshe kwa wakati ili kuviwezesha vikundi vingine vinavyohitaji kukopa.

"Huu mkopo hauna riba fanyeni shughuli zenu za ujasiriamali mjikwamue kiuchumi na kurejesha fedha hizo mlizokopa kwa wakati uliopewa, sio ombi ni lazima!" amesema Chaula.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Asia Ngalisoni amesema vikundi vya kata 14 kati ya 18 za wilaya hiyo vimenufaika na mkopo huo.

Kata hizo ni Orkesumet, Mirerani, Loiborseret, Langai, Edonyongijape, Ngorika, Msitu wa Tembo, Emboreet, Shambarai, Naberera, Terrat, Komolo na Oljoro namba 5.

Pia Soma

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Yefred Myenzi amesema vikundi 71 vya wanawake 59, vijana tisa na walemavu watatu vimepatiwa mkopo huo.

Naye mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck amewataka wanawake, vijana na walemavu kuchangamkia fursa hiyo inayotolewa na halmashauri hiyo.

Mmoja kati ya vijana waliopata mkopo huo, Zephania Lebahati amesema wamejinufaisha na ujasiriamali wa mifugo na kupitia mikopo hiyo watanufaika zaidi kiuchumi.

Chanzo: mwananchi.co.tz