Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chato mwanzo, mwisho wa JPM

D3e6d56fbba4c04038933c064e224092 Chato mwanzo, mwisho wa JPM

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VILIO, huzuni na simanzi vimetanda katika mitaa ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, mahali alikozaliwa Dk John Magufuli wakati mwili wake ulipokuwa ukipitishwa kwa mara ya mwisho ukitokea jijini Mwanza.

Itakumbukwa kuwa ni Januari mwaka huu, Rais Magufuli alikuwa hapa na wananchi walisikika wakilia huku wakisema aliwaahidi angekuja tena Aprili mwaka huu, lakini amerudi hazungumzi tena.

Chato ndio mjini ambao Dk Magufuli alikuwa mtu wao maarufu tangu alipokuwa mbunge wao kwa miaka 15, kati ya miaka 20 ya ubunge kwani miaka mingine mitano alikuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo.

Haikushangaza kuona maelfu ya wananchi wake walisubiri kwa hamu kuona kama kweli yaliyotangazwa usiku wa Machi 17, mwaka huu ni ya kweli kwamba Rais Magufuli amefariki dunia.

Katika eneo maarufu la Muungano kilipo kituo cha daladala cha zamani, mwili ulipitishwa hapo jana saa 12.00 jioni ukitokea jijini Mwanza ukipita katika miji kadhaa ikiwamo Katoro na kuingilia katika njiapanda ya Bwanga na kupita katika barabara hiyo ya kuingia mjini Chato katika eneo hilo maarufu.

Wakati mwili ulipofika Muungano, umati mkubwa wa watu wa rika zote walikuwa wamebeba majani ya miti huku wengine walitandika kanga barabarani ili mradi kuomboleza wakati mwili wa mpendwa wao ukipita.

Vilio vilisikika, watu wakilia huku wengine wakishindwa kuvumilia na kutaka kugusa jeneza, lakini watu wa ulinzi na usalama walihakikisha hakuna mtu anadhurika.

Waombolezaji wengine walisikika wakisema ‘ulituahidi utarudi, sasa umerudi ukiwa ndani ya jeneza,’ wengine walitamani anyanyuke na kuzungumza nao alicholenga kuwaambia Aprili mwaka huu, lakini haiwezekani tena.

Wanawake wamejilaza chini pembezoni mwa barabara wakilia kwa uchungu mkubwa. Watoto nao walikuwa wakilia, vijana nao hawakunyamaza.

Maduka, migahawa, magenge vyote vilifungwa ili kuwawezesha watu kushiriki maombolezo hayo. Bodaboda nazo ziliunga msafara nyuma ya magari ya Polisi huku vijana wakikimbia kuelekea msafara wakiimba, ‘Jeshi Jeshi…Magu Magu.

’ “Yule baba alikuwa mkarimu sana, akifika hapa alikuwa lazima asimame hapa njiapanda anatusalimia, anaenda.

Tutakukumbuka kwa mengi, ametujengea shule, hospitali na alituhimiza kufanya kazi,” alisema Martha Lutelemla, mjasiriamali mwenye mgahawa Muungano, eneo la makutano ya taa za kuongoza magari ambalo ni maarufu hapa.

Jana pamoja na ulinzi wa kawaida, pia helikopta mbili zilionekana zikizunguka angani kuimarisha ulinzi. Shughuli za maandalizi ya kuaga mwili zilikamilika jana na leo wananchi wa hapa watapata muda wa kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao katika Uwanja wa Magufuli.

Uwanja huu ulijengwa na Rais Magufuli kwa ajili ya mpira wa miguu na ujenzi ulikuwa ukiendelea. Dk Magufuli ambaye atazikwa kesho Ijumaa nyumbani kwake kijijini Rubambangwe wilayani hapa, mwili wake ulihifadhiwa nyumbani kwake baada ya kuwasili jana jioni.

Akizungumza jana usiku hapa, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi wananchi kutoka maeneo ya jirani na Chato wameombwa kujitokeza kwa wingi kuja katika Uwanja wa Magufuli kumuaga mpendwa wao.

Alisema wakati wa kutoa heshima za mwisho serikali imetoa nafasi maalumu kwa ajili ya makundi maalumu kuaga wakiwemo wasanii na waandishi wa habari.

Aidha, alisema kesho kama ilivyopangwa ataongoza waombolezaji kumuaga na kisha maziko ya mzalendo wa kweli, na kesho itak

Chanzo: www.habarileo.co.tz