Same. Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Mkomazi mkoani Kilimanjaro Tanzania, Abel Peter, amesema tembo waliovamia maeneo ya Same na kusababisha uharibifu wa mazao na kifo cha mtu mmoja wanatokana na baadhi ya wananchi kuwazingira wanyama hao na kuanza kuwapigia honi za bodaboda jambo lililoibua hasira kwa wanyama hao.
Akizungumza na Mwananchi jana Alhamisi Julai 4, 2019, Peter alisema tembo hao ambao walikua wawili, walitoroka katika hifadhi ya Mkomazi na kuingia kwenye maeneo ya wananchi ambapo mbali ya kusababisha kifo, walimjeruhi mtu mmoja na kusababisha uharibifu wa mazao, ambayo tathimini yake haijafanyika.
Alisema kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya hiyo kupitia kikosi cha Ujangili, wamefanikiwa kuwarudisha wanyama hao hifadhini juzi na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kuwa hali ni shwari.
“Kihistoria huwa wanyama hawa wanakuwa na mapito yao ya kupita na huu ndio msimu wao kutokana na mazao yaliyopo mashambani kwa sasa, lakini wananchi wamelima kwenye mapito yao na wakipita wanawafukuza na kuwapigia kelele.”
“Hii ni hatari na ndiyo husababisha wanyama hao kukasirika na kufanya uharibifu, kwani kawaida yao huwa hawapendi kelele,” alisema Peter
Kamishna huyo alisema tayari wamekutana na uongozi wa wilaya hiyo, kuweka mikakati ya kutoa elimu kwa wananchi ili kuchukua tahadhari pindi wanapowaona wanyama hao ili kuhakikisha hawawasogelei wala kuwapigia kelele.
Pia Soma
- Waziri wa Misri aahidi ushirikiano ujenzi mradi wa umeme Rufiji
- Raia, jeshi Sudan waafikiana uongozi wa mpito
- IGP Sirro azungumzia mauaji ya raia tisa wa Watanzania
- Alichokisema hakimu kesi ya vigogo wa Chadema
Kamanda Issah alimtaja aliyefariki ni Hansi Edes (47) mkazi wa Mheza kata ya Maore na kueleza kuwa tayari hali ya usalama imerejea katika eneo la Same baada ya tembo waliokuwa wamezagaa kurudishwa hifadhini.