Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa limesema basi la Kampuni ya New Force limepinduka katika mlima Kitonga wakati likikwepa kugongana uso kwa uso na basi jingine la kampuni hiyo.
Akizungumza leo Jumanne Oktoba 16, 2018 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Deusdedit Kashindo amesema kufuatia ajali hiyo watu 12 wamejeruhiwa, kwamba polisi wanamshikilia mmoja wa madereva wa mabasi hayo kwa uzembe.
Amemtaja dereva anayeshikiliwa kuwa ni Ramadhan Salmin aliyekuwa akiendesha basi lenye namba za usajili T623DNG lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya.
Dereva huyo anadaiwa wakati akilipita gari alikutana uso kwa uso na basi jingine la kampuni hiyo lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam.
“Wakati huo (akilipita gari hilo) basi lenye namba za usajili T852 DHA pia la kampuni ya New Force aina ya Hong Zong likkawa likawa linakuja mbele yake na katika kukwepa kugongana uso kwa uso lilipinduka na kuingia katika korongo refu na kusababisha watu 12 kujeruhiwa,” amesema.
Amesema miongoni mwa majeruhi ni dereva wa basi lililoanguka katika korongo na mtoto mwenye umri wa kati ya mwaka mmoja na miwili.
Amesema kati ya majeruhi hao, saba ni wa wanaume na watano wanawake na kwamba wanapatiwa matibabu katika hospitali teule ya Wilaya ya Kilolo.
Amebainisha kuwa majeruhi mmoja hali yake ni mbaya na amepelekwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Amefafanua kuwa dereva huyo atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.