WATENDAJI wa huduma za hoteli jijini Mbeya wamepongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha nchi kupata chanjo ya kujikinga na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Uviko-19 na kurejesha hali nzuri kibiashara katika sekta ya utalii na uwekezaji.
Wamesema hatua hiyo imewezesha kuondoa athari zilizojitokeza kutokana na mlipuko huo na sekta ya utalii kwa ujumla ikiwamo hoteli na nyumba za kulala wageni kuathirika kwa kukosa wageni.
Wamiliki hao walisema hali hiyo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na kundi la waandishi wa habari zaidi ya 30 wanaofanya ziara ya kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji nchini wakimsapoti Rais Samia katika kutangaza vivutio hivyo.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Usungilo ambao pia ni wamiliki wa Hoteli ya Usungilo, Kata ya Forest jijini hapo, Hotman Nyagawa, alisema ujio wa chanjo ya Uviko-19 imewezesha sekta ya utalii kuanza kurejea katika hali yake ya kawaida kwa upatikanaji wa wateja.
"Mwaka 2020/21 sekta ya utalii ikiwamo hoteli na nyumba za kulala wageni tuliathirika kwa kiasi kikubwa, hali ilikuwa mbaya hatukuwa tukipokea wageni pia sisi kwa sisi tulikuwa tunaogopana, tunamshukuru sana Rais, Samia kwa kuwezesha nchi kupata chanjo watu wamechanga na hivi sasa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida," alisema.
Alisema kwa sasa angalau wanakusanya japo asilimia 30 ya mapato tofauti na wakati wa corona walilazimika kufunga kutokana na biashara kuwa mbaya.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Hoteli Desderia, William Jima, alisema wameweza kuchangia katika sekta ya utalii kwa kuajiri asilimia 98 ya vijana kutoka Mkoa wa Mbeya na nje ya mkoa huo.
Kuhusu athari za Uviko-19 alisema waliathirika kwa kiasi kikubwa baada ya mlipuko huo, lakini kwa sasa hali imebadilika na wageni wameanza kuingia kama kawaida.
"Nawashauri watu wakachanje ili maisha yaweze kuendelea kwani ukichanja unakuwa umejikinga na mlipuko wa Uviko-19, tusipuuze kuchanja maana ni kawaida yetu, japo kuchanja ni hiari," alisema.
Hivi karibuni Rais, Samia amezindua kampeni ya kuchanja kwa hiari inayoendeshwa nchi nzima na kila wizara sambamba na kutoa mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa ajili ya mapambano dhidi ya Uviko-19 na kupunguza athari zilizotokana na ugonjwa huo.