Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Changamoto ya kuhifadhi maiti inavyoumiza vichwa Kilwa

60135 MOCHWARI+PIC

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Inapotokea jamii fulani ikaondokewa na mpendwa wao ndugu, jamaa na marafiki hukusanyika pamoja na kuaga mwili kabla ya kuupumzisha kwenye nyumba yake ya milele.

Hili halikufanikiwa kwa Joseph Japhet ambaye alishindwa kuaga mwili wa baba yake mzazi Juni mwaka jana, kwa kukosekana mahali pa kuuhifadhi ‘mochwari’.

“Nilipokea simu kuwa baba amefariki ilikuwa ni ghafla na wala hakuumwa ila ni presha, wakati huo nilikuwa kazini (Singida) mida ya saa 10 jioni ilikuwa vigumu kuanza safari muda huo. Ilinichukua zaidi ya saa 24 kufika Kilwa. Nasikitika nilikuta kaburi kwani ilikosekana nafasi kuhifadhi mwili,” anasimulia Joseph.

Yeye ni miongoni mwa waathirika wa kukosekana kwa huduma ya kuhifadhi maiti katika Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi ambako zahanati (52), vituo vya afya (5) na hospitali (2) vyote vinakitegemea chumba kimoja chenye jokofu moja lenye uwezo wa kuhifadhi maiti mbili tu kwa siku.

Hata hivyo, bado jiografia yake si nzuri kwani mgonjwa afikapo tu hospitalini hapo ni lazima akutane na mochwari ndipo alifikie jengo la kuona wagonjwa (OPD) hali ambayo kisaikolojia si rafiki kwa mgonjwa.

Wenyeji wa mji mkongwe wa Kilwa Masoko wanasema chumba hicho kilichojengwa mwaka 1964 ndicho kinachotegemewa mpaka sasa.

Pia Soma

Changamoto

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilwa, Abuu Mchau anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema kuwa tangu ilipojengwa haijawahi kufanyiwa marekebisho.

“Jokofu lililopo kwenye chumba chetu cha kuhifadhia maiti ni bovu, tulilitengeneza mara ya kwanza likafanya kazi kwa miezi kadhaa likaharibika ikafikia hatua tunaona gharama za kulitengeneza ni kubwa ni bora kuwa na chumba kingine cha kuhifadhia maiti,” anasema.

Anasema kutokana na changamoto hiyo kuzidi, walishauriana na mkurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanatafuta suluhu, hivyo waliiomba Kampuni inayojihusisha na uchakatuaji na uuzaji wa gesi asilia Pan African Energy (PAET) iwajengee chumba kingine na mahitaji mengine ya halmashauri hiyo.

“Hii ni hospitali ya wilaya na hii ni barabara kubwa ya Mtwara-Dar inaweza kutokea ajali kimbilio letu kubwa ni pale na tunashindwa kuhifadhi maiti kwa sababu jokofu hatuna.

“Mara nyingi tunashidnwa kuhifadhi maiti pale, inafikia hatua hupata wakati mgumu hata watumishi wetu wanaofariki taratibu zetu za kuaga tunashindwa kuzitimiza.”

Alipoulizwa kuhusu eneo ilipo mochwari hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) Dk Khalfanis Ilekizemba anasema hospitali hiyo ilipojengwa mwaka 1964 chumba hicho kilikuwa eneo la nyuma lakini njia ya kuingilia ilipobadilika chumba hicho kikawa mbele.

Hata hivyo, anasema “tunalo jokofu moja linatunza maiti mbili kwa wakati mmoja lakini hakuna sehemu ambayo maiti itafanyiwa uchunguzi, hatuna jokofu la kisasa pia ipo eneo la mbele wagonjwa wanakata tamaa mapema wanapokuja kutibiwa na kukutana kwanza na mochwari.”

Anasema kwa wastani hospitali hiyo hupokea maiti 16 hadi 18 kwa mwezi, “hivyo unapoboresha huduma pia mahitaji yataongezeka, hatutarajii kuhifadhi maiti bali watu wapone, lakini ikitokea maafa tutashindwa namna ya kuhifadhi.”

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa Renatus Mchau alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo akisema kwa wastani wanaohudumiwa na hospitali hiyo ni karibu watu 200,000 huku ikihudumia wagonjwa 1,000 mpaka 2,000 kwa siku.

Ufadhili wapatikana

Mchau anasema baada ya kutafuta ufadhili, PAET imewapatia Sh1.241 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya afya huku Sh161 milioni zikielekezwa katika ujenzi wa mochwari.

Anasema Sh838 milioni zitajenga kituo cha afya Somanga, Sh161 chumba cha kuhifadhia maiti na Sh242 milioni zitajenga duka la dawa katika hospitali ya wilaya.

“Wilaya tumepanga tuwe na mochwari kubwa zaidi na ya kisasa ikilinganishwa na ile iliyopo. Itagharimu Sh161, itakuwa na jengo la kisasa lenye jokofu la kulaza maiti nne, chumba cha uchunguzi, kuoshea maiti na ofisi,” anasema.

Anasema mkakati uliopo ni vituo vipya vinavyojengwa vikiwamo vya Kilwa Masoko, Pande, Nanjilinji na kipya cha Somanga kila kimoja kitakuwa na vyumba vya kuhifadhia maiti.

Chanzo: mwananchi.co.tz