Dar es Salaam. Chama cha Wachapishaji Tanzania (Pata) kimeeleza changamoto tatu zinazokikwamisha na kuiomba Serikali ya Tanzania kuzifanyia kazi ili kukuza sekta ya uchapishaji nchini humo.
Moja ya changamoto hizo zilizoainishwa na mwenyekiti wa chama hicho, Gabriel Kitua ni kutokuwa na sera ya kitaifa ya vitabu inayobainisha matarajio na majukumu ya wadau mbalimbali katika mlolongo wa uundaji, usambazaji na utumiaji wa vitabu.
Nyingine ni utekelezaji wa vitendo wa sera ya elimu ya kujifunza na ufundishaji shirikishi na kuchelewa upatikanaji wa ithibati kwa vitabu vya ziada.
Akizungumza wakati akikabidhi msaada wa vitabu 30,0500 katika maktaba Kuu ya Taifa vyenye thamani ya zaidi ya Sh100 milioni, leo Jumatano Agosti 28,2019 amesema lengo la msaada huo ni kuongeza ufanisi wa maktaba hiyo kuwa na vitabu vya kutosha vitakavyoongeza maarifa na uelewa kwa jamii.
Kuhusu utekelezaji kwa vitendo wa sera ya elimu ya kujifunza na ufundishaji shirikishi amesema itafanikiwa endapo kutakuwa na vitabu vya kutosha na kubainisha kuwa kuna uhaba wa vitabu katika maktaba nchini.
“Tunaelewa kuwa maktaba zina mchango mkubwa ila changamoto ni kwamba zipo chache na zina uhaba wa vitabu kwa hiyo tunatarajia wenye shule iliwemo Serikali watahakikisha kuwa kila shule inakuwa na maktaba na zinakuwa na vitabu vya kiada na ziada vya kutosha,” amesema
Pia Soma
- Trump akandia waandishi kuandika 'mafuriko' ya kampeni za mpinzani
- Wakazi wa mji wa Mtwara kuendelea kusota na mgao wa maji
- Kikongwe aliyepigania ardhi yake kwa miaka 42 kulipwa milioni 500
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo mkurugenzi mkuu wa maktaba ya Taifa, Dk Alli Mcharazo amesema vitabu hivyo vitaziba pengo la uhaba wa vitabu hasa kwa lugha ya Kiswahili.