Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chalamila ataka waliounguliwa maduka wakopeshwe fedha

Moto Mwenge Fedha.png Chalamila ataka waliounguliwa maduka wakopeshwe fedha

Tue, 5 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameutaka uongozi wa Wilaya ya Kinondoni, kukutana na wafanyabiashara 32, ambao bishara zao zimeteketea, kufuatia moto uliotokea eneo la Mwenge, kuangalia namna ya kupata fedha za kuwakopesha.

Katika kikao hicho, RC Chalamila ametaka kihusishe kutafuta njia mbadala ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuwakopesha wahanga hao ili waendelee na shughuli zao.

Hata hivyo, Chalamila amesisitiza kufanyika kwa uchunguzi dhidi ya tukio hilo na kama kuna hujuma zozote, hatua za kisheria zichukuliwe.

Chalamila ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Desemba 5, 2023 alipozungumza na wananchi baada ya kuwasili katika eneo la tukio.

Amesema kikao cha uongozi wa wilaya hiyo na wafanyabiashara kinapaswa kufanyika haraka na itafutwe fedha kwa ajili ya mikopo kwa wahanga.

"Uongozi wa Kinondoni ni muhimu kukaa na wafanyabiashara 32 ili kuangalia njia ya haraka na kama kuna fedha za kuwakopesha, wapewe ili walipe kwa riba kidogo," amesema.

Kwa maoni yake, Chalamila anadhani kwamba japokuwa vyanzo vya moto katika maeneo kama hayo hutokea kwa bahati mbaya, lakini pia inaweza kuwa ni uhalifu ulioratibiwa au uzembe na hapa ndipo penye mantiki ya kuhitaji uchunguzi ufanyike.

Chalamila anataka uchunguzi huo ufanyike kwa muda mfupi ili kubaini chanzo cha moto huo, huku akisema kuwa kutokana na tukio hilo, imebainisha wazi ni kwa namna gani wafanyabiashara hawajui thamani ya benki.

"Wafanyabiashara wengi hawajui thamani ya benki kwani ndani ya moto kiasi kikubwa ya fedha kimeshuhudiwa kikiteketea," amesema.

Kadhalika, ametaka uongozi wa wilaya hiyo, kujipa miezi sita kwa ajili ya ujenzi wa ene hilo ili kuepuka matukio kama hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema eneo hilo lilikuwa na fremu 32 na biashara 30.

"Moto umeteketeza rasilimali na bidhaa zilizokuwepo ni hasara kwa mapato, ajira na kodi ambazo Serikali inafaidika nazo," amesema.

Amesema tayari timu ya uchunguzi inayohusisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na wataalamu wa Ardhi imeundwa kubaini chanzo cha moto huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live