Chama cha Wananchi (CUF), kimeeleza kuwa kimejipanga kurejesha heshima yake visiwani Zanzibar, ifikapo 2025 kwa kuunda Serikali au kushiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hayo yamesemwa jana tarehe 16 Januari 2023 na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF, Mhandisi Mohamed Ngulangwa, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, kuhusu kauli iliyotolewa na Chama cha ACT-Wazalendo, kwamba kimekufa.
“Nataka nikuhakikishie, hakutakuwa na ACT-Wazalendo kwenye Serikali ijayo, maana yake CUF kama hatukuchukua Serikali Zanzibar, tutakuwa tunaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” amesema Mhandisi Ngulangwa.
Mkurugenzi wa Uenezi CUF, amesema kuwa chama chake kimeendelea kujiimarisha visiwani Zanzibar na Bara, na kwamba wanachama wake waliokimbilia ACT-Wazalendo kuanzia 2019, wameanza kurejea nyumbani.
“Mipango yetu tunaendelea nayo na tulikuwa tunaitumia mikutano ya hadhara, mwaka huu tunakamilisha uchaguzi wa ndani ya chama ikifika Oktoba tutapata safu ya uongozi itakayotusaidia kufanya vizuri katika chaguzi zijazo,” amesema Mhandishi Ngulangwa.