Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo, Sharifa Nabalang'anya kufanya uchunguzi wa matumizi ya Sh12.5milioni zilizotolewa na halmashauri hiyo kwa ajili ya umaliziaji wa darasa la Shule ya Msingi Idibo baada ya wanakijiji kuingiwa na shaka kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi katika kata za wilaya hiyo, leo Jumatatu Machi 25, 2024, Mwenyekiti wa CCM Wilayani Gairo, Dunstan Mwendi amesema shaka lililowaingia wananchi juu ya matumizi ya fedha hizo ni katika umaliziaji wa chumba cha darasa.
Hivyo, Mwendi ameitaka ofisi ya mkurugenzi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwaondolea shaka wananchi hao.
Amesema malalamiko hayo ya wananchi yanapaswa kufanyiwa kazi ili kujiridhisha kwa tuhuma hizo na endapo itaonekana kuna ubadhirifu wa matumizi mabaya ya fedha za umma, lazima sheria ichukue mkondo wake kwa kuwawajibisha wote waliohusika.
“Nikuagize Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Gairo, (Petronilla Wakurila), ofisi yenu ifanye uchunguzi wa madai ya matumizi ya hizi fedha kwa sababu Serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, tunataka fedha zifanye kazi zilizokusudiwa,” amesema Mwendi.
Katika mkutano huo, mkazi wa kijiji hicho, Charles Mhando (60) amesema wananchi wa Idibo wamejitolea kujenga chumba cha darasa la awali la shule hiyo kuanzia msingi hadi kupaua.
“Tumepata taarifa kuwa shule ya msingi Idibo imepokea Sh12.5 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ilhali sisi tumetumia nguvu zetu kujenga chumba cha darasa la awali kuanzia msingi hadi kupaua, sasa hizo fedha zimetumika katika ujenzi upi?”amehoji Mhando.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Gairo, Petronilla Wakurila amesema halmashauri imetoa Sh12.5 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa darasa hilo ikiwa ni muendelezo wa maboresho ya sekta ya elimu msingi na sekondari.
“Hizi fedha zimekuja kwa ajili ya kujenga darasa hili la shule ya awali,” amesema Wakurila.