Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Tanga imejitosa katika vita dhidi ya dawa za kulevya ikiwataka wanachama wake ngazi ya mashina, kuhakikisha mkoa huo hauwi lango la walanguzi wa dawa za kulevya.
Kauli hiyo ya CCM imetolewa na Mwenyekiti wake mkoani hapo Rajab Abdurahman wakati akizundua mashina mapya ya chama hicho.
"CCM ina vijana imara lazima uimara wenu muonyeshe katika kuisaidia Serikali na vita dhidi ya dawa za kulevya hasa uuzaji na utumiaji,usafisheji mkoa huu sitaki nisikie Tanga ndio lango la walanguzi wa dawa za kulevya,"ameaema.
Abdurahman amesema lazima vijana wa chama hicho wasimame kidete kuusafisha mkoa huo dhidi ya watu wachache wanaoujengea mkoa huo taswira mbaya.
"Mashina haya nane yenye waendesha bodaboda na wajasiriamali vina uwezo wa kuwa vituo vikubwa vya kuzuia na kukomesha biashara haramu,"amesema.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ametoa maagizo kwa askari wa Jeshi la Polisi kuacha kuwanyanyasa vijana wanaoendesha Bodaboda kinyume cha sheria.
"Siungi mkono uvunjifu wowote wa sheria utakaofanywa na Jeshi la Polisi niwaombe wafanye kazi kwa uweledi wasiwaonee raia," amesema.
Baadhi ya vijana katika vituo vya bodaboda wamesema kuwa maelekezo ya Mwenyekiti huyo watazingatia ili vijiwe vyao visiwe na dosari yoyote .