CHAMA Cha Mapinduzi wilayani Kaliua Mkoani Tabora kimempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Jerry Mwaga, kwa kutoa mikopo nafuu ya Sh mil 290 kwa vikundi 45 vya vijana, wanawake na walemavu ili kuwainua kiuchumi.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Katibu wa CCM wilayani humo, Salome Luhingulanya katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa huo Dk Philemon Sengati.
Alisema kuwa mikopo hiyo ambayo imetolewa kwa vikundi zaidi ya 45 vya wakazi wa wilaya hiyo ni ishara njema kwa Uongozi wa halmashauri hiyo katika kuhakikisha inatekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo.
Aidha alitoa wito kwa vikundi vyote vya vijana, akinamama na walemavu vilivyopewa mikopo hiyo kuitumia vizuri ili isaidie kuwaongezea kipato na kuinua maisha yao kiuchumi, aliwataka kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili na wenzao wapate.
Awali Mkurugenzi wa halmashauri hiyo alisema kuwa kiasi cha sh 290,000,000/- kinachotolewa kwa vikundi hivyo, sh 144,429,141 ni za mapato ya ndani, sh 139,570,858 ni marejesho ya mikopo na sh 6,000,000/- ni bakaa ya bajeti iliyopita.
Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo sh mil 119 zimekopeshwa kwa vikundi 23 vya wanawake, sh mil 156 kwa vikundi 17 vya vijana na sh mil 15 kwa vikundi 15 vya watu wenye ulemavu, vikundi hivyo vyote vimetoka katika kata zaidi ya 15.
Aidha alibainisha kuwa mbali na mikopo ya fedha taslimu pia wametoa jumla ya bodaboda 30 zenye thamani ya zaidi ya Sh 60,000,000 kwa vikundi vya vijana wa kata za Ushokola, Usinge na Ichemba ili kuinua maisha yao kiuchumi.
Akiongea katika hafla hiyo wakati wa kukabidhi hundi ya sh mil 290 na bodaboda 30, Mkuu wa Mkoa huo Dk Philemon Sengati aliipongeza halmashauri hiyo kwa kasi yao kubwa ya ukusanyaji mapato na kutekeleza agizo la serikali kwa vitendo.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani humo Mwanahamis Ally alieleza kuwa wameweka mkakati thabiti wa kuboresha utendaji kazi wa vikundi vyote ili kuviimarisha zaidi na kuhamasisha uundwaji vikundi vyenye mlengo wa kuanzisha viwanda vya uzalishaji mali ili kunufaisha wakazi wa wilaya hiyo, mkoa na taifa kwa ujumla.