Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CAG anusa ufisadi Feri Dar

1f52d1701bb26f756ce76a926180e74d.jpeg CAG anusa ufisadi Feri Dar

Fri, 9 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini kuwepo kwa viashiria vya ubadhirifu katika Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA).

Katika ripoti yake ya mwaka wa fedha 2019/20 aliyowasilisha bungeni jana, CAG alibaini makusanyo ya kivuko cha Magogoni kiasi cha Sh milioni 81.1 hayajapelekwa benki na hayapo kituoni.

“Nilibaini kuwa Kituo cha Kivuko cha Magogoni kilikusanya jumla ya Sh bilioni 5.757 ikiwa ni tozo za kivuko kwa kipindi kilichoanzia Julai 2019 hadi 30 Juni 2020. Hata hivyo, kati ya fedha zilizokusanywa, ni Sh bilioni 5.675 ndizo zilizowekwa kwenye akaunti ya benki inayosimamiwa na Makao Makuu ya TEMESA,” alisema CAG.

Alisema alibaini kiasi hicho cha fedha ambacho hakikuwekwa benki pia hakikuwa kwenye himaya ya kituo.

“Kwa maoni yangu, fedha hizi ambazo hazijawekwa benki kuna uwezekano kwamba zimetumiwa vibaya au kutumiwa katika shughuli zingine,” alisema.

Alisema mfumo usio madhubuti wa tiketi za Kielektroniki katika Kituo cha Feri cha Magogoni – Sh. bilioni 2.594 alibaini kuwa Temesa iliuza jumla ya tiketi 21,447,004 zenye thamani ya Sh bilioni 5.76.

Hata hivyo, alisema ni tiketi 9,122,690 tu zenye thamani ya Sh. bilioni 3.16 ndizo zilizothibitishwa na mashine huku tiketi 12,324,314 zenye thamani ya Sh. bilioni 2.60 zikitumika bila ya kuthibitishwa na mashine.

“Ni maoni yangu kuwa, tiketi hizo zinaweza kutumika tena na kusababisha serikali kupoteza mapato,” alisema.

Aidha, alisema ukaguzi maalumu aliofanya katika Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi alibaini fedha kwa ajili upangaji wa ardhi zilizotumika kinyume cha malengo Sh milioni 69.04.

“Ukaguzi wangu ulibaini kuwa Tume ilifadhili matumizi ya mkutano wa Bodi ya Mkurugenzi kwa gharama ya Sh 69,041,415.46 kutoka kwenye fedha zilizotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais ili kutekeleza shughuli za upangaji matumizi ya ardhi katika wilaya za Nyasa, Mbinga, Ludewa, Makete na Kyela,” alisema.

Pia alisema mapungufu yaliyoibuliwa kwenye usimamizi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), alibaini mmoja wa maofisa wa tume hiyo alitumia Sh milioni 5.63 ambazo hazikuwa kwenye bajeti.

Pia alisema Sh milioni 5.58 zilitumika zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa na mmoja wa maofisa bila idhini ya Mkurugenzi Mkuu.

“Pia, nilibaini kuwa kiasi cha Sh milioni 8.56 zilichukuliwa na mmoja wa wafanyakazi wa Tume kwa kutekeleza shughuli za upangaji wa matumizi ya ardhi katika vijiji 10 vya Wilaya ya Chato kwa kudanganya idadi ya siku zinazostahili kulipwa kwa walengwa waliohudhuria mafunzo,” alisema.

Kuhusu kughushi nyaraka za malipo Sh milioni 160.78, alisema alibaini kuhusu kughushi nyaraka za malipo ikiwamo maofisa sita katika wilaya saba walighushi saini za walengwa na kujipatia jumla ya Sh milioni 38.16.

“Pia, nilibaini ushirikano kati ya wafanyakazi wanne kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, mmoja kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na wawili kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi ambao walidanganya siku za malipo na kujipatia kiasi cha shilingi milioni 61.65,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz