Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bweni la wavulana lateketea kwa moto Chalinze

Bweni Pic Data Bweni la wavulana lateketea Chalinze

Tue, 5 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Moto umezuka ghafla katika Shule ya msingi ya Wavulana ya Chalinze Modern Islamic Mkoa wa Pwani nchini Tanzania na kuunguza bweni la Wavulana pamoja na kuteketeza vifaa mbalimbali vya wanafunzi ikiwemo nguo na madaftari.

Moto huo umezuka leo Jumanne Julai 05, 2022 wakati wanafunzi wa bweni hilo wakiwa kwenye Ibada Msikitini kwenye eneo hilo.

Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo, Abubakar Kunenge amethibitisha tukio hilo na kueleza hakuna madhara ya kiafya na maisha yaliyotolewa kwa wanafunzi shuleni humo.

"Ni kweli tumepata changamoto ya tukio la moto katika Shule ya Chalinze Isalmic Modern school lakini tunamshukuru Mwenyezi Mungu hatukupata madhara yanayohusisha athari za kiafya na maisha ya wototo wetu," amesema Kunenge na kuongeza:

"Hakuna vijana walioumia, hakuna madhara ya vifo na vijana wetu wataendelea na masomo kama kawaida," amesema

Ametaja vitu vilivyoteketea ni nguo za shule, mabegi, sabuni na baadhi ya madaftari walivyokuwa wakikaa navyo kwenye hilo

Kunenge amesema shule hiyo ina majengo mengi hivyo  wanafunzi ambao bweni lao limeungua wamepata mahali pengine pa kulala.

Kunenge amelishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani hapo kwa Elimu wanayotoa kwa Shule za Mkoa huo katika udhibiti wa moto kwani imesaidia kwenye tukio hilo na kutoa rai kwa Shule zote  kupata mafunzo ya elimu jinsi ya kuthibiti madhara ya moto hatua za awali,

"Shule hii ilipokea mafunzo mwezi mmoja uliopita na moto huo ulipotokea vijana na Jumuiya ya Wafanyakazi wa shule hii wamethibiti moto huu kutumia vizimia Moto (Mitungi) kabla gari la zimamoto halijafika na ni kutokana na kupata mafunzo" amesema Kunenge

Mkuu huyo wa Mkoa amesema tayari ameunda timu ya kitaalamu ya kuchunguza chanzo cha moto huo ambao bado hakijafahamika

Naye Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani Jenipher Shirima amesema moto huo ulizuka alfajiri ya Julai 05 saa 11:42 .

Shirima amesema moto huo umefanikiwa kudhibitiwa mapema kupitia vizimia moto vilivyopo shuleni hapo.

"Kutokana na changamoto ya matukio kama haya ya moto mashuleni Jeshi letu lipo kwenye program ya utoaji mafunzo  katika  shule za msingi na sekondari mkoani kwetu," amesema Shirima

Awali, Mkurugenzi wa shule hiyo ya Chalinze Modern Islamic Omary Ismail amesema bweni lililoathirika ni la wavulana na  vifaa vya wavulana nane ndiyo vimeteketea vyote.

Ismail ameshukuru kwa mafunzo ya Jeshi la zimamoto yaliyotolewa hivi karibuni hapo kwani vimewawezesha kuzima moto huo kwa muda mfupi kabla Jeshi la Zimamoto na uokoaji hakijafika eneo la tukio

Chanzo: www.mwananchi.co.tz