Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bweni Sekondari ya Ufundi Kengeja lateketea, wanafunzi wanusurika

Bweni Mptooo.png Bweni Sekondari ya Ufundi Kengeja lateketea, wanafunzi wanusurika

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wanafunzi wa kiume wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Kengeja wamenusurika kifo baada ya bweni kuungua moto usiku wa kuamkia leo, wakati hao wakiwa wamelala.

Moto huo ulioanza kuwaka saa tisa usiku, umeteketeza vitu vyote vilivyokuwamo kwenye bweni hilo ambavyo ni vitanda,makabati, madaftari na vitu vyingine.

Ajali kama hiyo iliwahi kutokea kwenye shule hiyo Mei 22 mwaka 2022, bweni la wanawake liliteketea kwa moto kutokana na hitilafu ya umeme na kusababisha hasara.

Akizungumza na Mwananchi Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Zanzibar, Khamis Abdalla Said amesema tukio hilo lilitokea usiku wa manane na kuharibu mali mbalimbali za shule pamoja na wanafunzi.

Amesema wakati moto huo unatokea kwenye bweni hilo hakukua na wanafunzi wengi baada ya baadhi yao kurudishwa nyumbani kutokana na ugonjwa wa macho (red eyes).

Amesema kwa sasa wanaendelea na jitihada kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo wanapata sehemu nzuri ya kukaa na kuendelea na masomo yao.

‘’Tayari tumeshaandika barua kwa mamlaka husika kutaka utafiti wa kina ufanyike kwenye shule zote za bweni mpya na kongwe kutazama mifumo ya umeme iliyopo inawezekana kukawa na tatizo ambalo sisi hatuwezi kuligundua,’’amesema.

Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Khamis Hamad Haji amesema moto huo uliwaka usiku mkubwa na hakuwa na uwezo wowote wa kupambana nao.

Amesema walichokifanya ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayedhuriwa na moto huo na watoto wote walitoka wazima.

Baadhi ya wanafunzi hao wameiambia Mwananchi kuwa, walishtushwa baada ya kusikia kelele kubwa kutoka kwa wenzao na kuwataka watoke haraka ndani.

‘’Sisi tulijua kutoka tu ndani, hatukuweza kukumbuka lolote lile,’’amesema mmoja wa wanafunzi hao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor amesema wameamua kuwarudisha nyumbani wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu mpaka Ferbruari 4 2024.

Amesema lengo ni kuwapunguzia hofu wanafunzi hao pamoja na wazazi wao waliopatwa na mshtuko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live