Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bwawa la mgodi wa Mwadui labomoka, wananchi wakimbia makazi

Bawa PicHNH Bwawa la mgodi wa Mwadui labomoka, wananchi wakimbia makazi

Tue, 8 Nov 2022 Chanzo: mwanachidigital

Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui wilayani Kishapu, limepasuka na kutiririsha tope na kuelekea kwenye makazi ya watu na mashambani, hali iliyosababisha wananchi kukimbia makazi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa simu leo Novemba 8, Ofisa Uhusiano wa mgodi huo, Bernard Mihayo amesema tukio hilo kweli limetokea, lakini hawezi kuzungumzia suala atalizungumzia Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumzia tukio hilo leo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema amesema janga hilo limesababisha nyumba 13 katika kijiji cha Ng’wang’olo kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu, kuingiliwa na maji.

Hata hivyo amesema hakuna mtu aliyepoteza maisha katika tukio hilo, ila kuna watu wazima wawili na watoto wanne waliokuwa wamepotea na sasa walipatikana baada ya wananchi kukimbia makazi yao.

Mjema amesema kutokana na janga hilo tayari ameshatuma kamati kukagua chanzo cha tukio hilo limesababishwa na nini, hivyo baada ya kuchunguza ndani ya siku saba italeta majibu.

"Tunawaomba wananchi waendelee kutulia wasiwe na taharuki, Serikali ipo pamoja nao inaendelea kufanya kazi yake.

“Wananchi walioacha chakula ndani ya nyumba zilizovamiwa na maji hayo mgodi wa WLD utawahudumia kwa kuwapa chakula na maji,” amesema.

Aidha amesema kutokana na tukio hilo mgodi umesimamisha shughuli zake ili kuhakikisha kuna usalama, baada ya hapo utaendelea na shughuli za uzalishaji.

Alipoulizwa kwa simu leo, Mkurugenzi mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira(NEMC), Dk Samuel Gwamaka amesema kuwa timu ya wataalamu wa baraza hilo ipo eneo la tukio kupima kiwango cha uharabifu kwa ushirikiano na Serikali ya mkoaa na mgodi.

“Lengo ni kuzuia maji yasisambae zaidi ilivyosasa, toka jana yamesambaa karibu kilomita nane.Uharabifu uliojitokeza ni pamoja na mashamba na baadhi ya nyumba kujaa matope, lakini tunaendelea kufanya tathimini,” amesema Dk Gwamaka.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Ng’wang’olo Kaya ya Mwadui, Luhumbo Kikuyu, akizungumza na waandishi wa habari ambao wamefika eneo la tukio, amesema baadhi ya nyumba za wananchi zimefunikwa na tope na wamekimbia kaya zao huku mashamba na visima vya maji vikifunikwa.

Kikuyu amesema kuwa bwawa hilo limepasuka jana Novemba 7 majira ya saa 4 asubuhi na kuanza kutiririsha tope zito na kuharibu makazi ya watu pamoja na mashamba yao.

Chanzo: mwanachidigital