Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bulembo ataja mafanikio, changamoto kliniki ya ardhi Kigamboni

Bulembo Pic Bulembo ataja mafanikio, changamoto kliniki ya ardhi Kigamboni

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

liniki ya kusikiliza changamoto za ardhi Kigamboni imehitimishwa leo Jumatatu, huku Mkuu wa wilaya hiyo, Halima Bulembo akisema jumla ya migogoro ya ardhi 316 imewasilishwa na wananchi wakitaka utatuzi.

Kliniki hiyo iliyokuwa na lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za ardhi ilianza Agosti Mosi mwaka huu, ikizinduliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba Maendeleo na Makazi, Dk Angelina Mabula katika Kata ya Mjimwema ambapo alipongeza ubunifu wa Bulembo katika mchakato huo.

Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu Agosti 28, 2023 Bulembo amesema kliniki hiyo iliyoambatana na watalaamu wa ardhi na mazingira ilikwenda katika kata zote tisa za Kigamboni, wamemaliza Kata ya Kigamboni akisema kati ya migogoro 197 kati ya 316 imepata ufumbuzi wa moja kwa moja.

"Lakini migogoro 124 bado inaendelea kushughulikiwa kwa sababu mtu anakuja binafsi na kutoa kero zake pasipo kuwepo na mtu anayemlalamikia, sasa jukumu letu ni kutafuta upande wapi na kuweka pamoja na kupata ufumbuzi.

"Lakini kuna wengine wamepeleka mashauri yao katika baraza la ardhi la wilaya na sababu nyingine inayochelewesha migogoro 124 kutokakamilika ni pamoja na nyaraka za walalamikaji kutokamilika," amesema Bulembo.

Bulembo aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga, amesema sababu za uwepo wa migogoro ya ardhi kuwa mingi wilayani humo ni pamoja baadhi ya wenyeviti na watendaji wa mitaa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na wasimamizi wa mirathi kuuza maeneo pasipo kushirikisha wanandugu.

Jambo jingine Bulembo amesema wananchi wengine hawana elimu kuhusu ardhi, ndio maana wanajikuta wakiingia katika migogoro ardhi hasa wanaopenda njia ya mkato pasipo kufuata utaratibu uliowekwa na halmashauri hiyo.Pia uwepo wa maeneo yasiyoendelezwa na kusababisha watu kuyavamia.

"Suala jingine ni urasimishaji ardhi unaofanywa na kampuni binafsi ambazo baadhi hazitekelezi mchakato huu kwa weledi. Sasa hili jambo limepata ufumbuzi ambapo manispaa tutaanza kupima wenyewe maeneo ili kupunguza changamoto.

"Kliniki hii siyo mwisho wa kusikiliza migogoro ya ardhi bali kila Alhamisi tutakuwa tunasikiliza kama ilivyo utaratibu wetu, lakini kama hiyo haitoshi tumekubaliana na watalaamu wangu kushuka katika mitaa kwenda kuwasikiliza wananchi wale waliokosa nafasi kutoa kero zao," amesema Bulembo.

Bulembo amesema katika kata tisa migogoro iliyojitokeza zaidi ni mirathi, watu kuuziwa kiwanja kimoja zaidi ya mara mbili wakishirikiana na viongozi wa mitaa husika.

Mmoja wa wakazi wa Kata ya Kigamboni, Elizabeth Sorogo amesema, "Tunamshukuru sana DC (Bulembo) na timu yake tumeongea vizuri na tumesikilizwa hasa migogoro ya mipaka, nilikuwa na mwingiliano wa mipaka na jirani lakini kupitia kliniki umekwisha hali ni nzuri.

"WanaKigamboni waje majibu ya changamoto zinazowakabili yapo, kama hakuna unapewa mwongozo wa namna ya suala litakavyoshughulikiwa .Watumishi wa Kigamboni wakiongozwa na Bulembo wamekuwa na ushirikiano katika suala hili nawashukuru," amesema.

Chanzo: mwanachidigital