Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bukoba Sekondari haikuzibwa ufa sasa wanajenga ukuta

32154 Pic+bukoba TanzaniaWeb

Tue, 18 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kengele ya tahadhari kuhusu udhaifu wa miundombinu ya shule ya sekondari Bukoba ilipigwa tangu mwezi Machi mwaka huu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa (RCC)baada ya mjumbe kuhoji fungu la ukarabati.

Katika kikao hicho Shekhe wa Mkoa wa Kagera Haruna Kichwabuta alihoji ilipo mifuko 200 ya saruji iliyotengwa ili kuikarabati tena Bukoba sekondari baada ya kutikiswa na tetemeko la ardhi la Septemba mwaka 2016 na majengo yake kubaki na nyufa.

Kiongozi huyo wa kiroho alionyesha hofu ya janga linalokuja kwa wnafunzi na walimu wa shule hiyo baada ya kuwepo kwa majengo yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi na kshauri ukarabati wa shule hiyo liwe jambo la kipaumbele.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Chibunu Lukiko alijibu hoja hiyo kwa kukieleza kikao kuwa mifuko ya saruji 200 iliyopokelewa kwa ajili ya ukarabati wa sekondari ya Bukoba ilihamishiwa sekondari ya Kagemu.

Hoja iliishia hapo na wanafunzi na walimu wao wakaendelea kutumia majengo hatarishi hadi hivi karibuni shule hiyo ilipofungwa kwa lazima baada ya majengo kuezuliwa na upepo mkali na kuwa katika hatari ya kuporomoka.

Shule ya sekondari Bukoba ilijengwa mwaka 1939 iliharibiwa na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Oktoba 17 mwaka huu ikiwa imeambatana na upepo mkali, na kubabisha mapaa yake kuezuka na maisha ya walimu na wanafunzi yangekuwa hatarini zaidi kama wangekuwa shuleni.

Uhamishoni Ihungo na Omumwani

Hatua ya dharura iliyochukuiwa na Serikali ni kuifunga shule hiyo na wanafunzi pamoja na walimu wao kuhamishiwa kwa muda usiojulikana katika shule za Ihungo na Omumwani ambazo zilikarabatiwa baada ya kuathiriwa na tetemeko.

Jumla ya wanafunzi 97 wa kidato cha tano na sita walipelekwa sekondari ya Omumwani na idadi kubwa ya wanafuzni 751 wa kidato cha kwanza nan ne kupelekwa sekondari ya Ihungo ambayo iko nje ya mji wa Bukoba.

Suala la umbali limeibua changamoto kwa idadi kubwa ya wanafunzi ambao sasa wanalazimika kutembea takribani kwa wastani wa kilometa nne kufika shuleni huku mji wa Bukoba ukiwa hauna magari yanayotoa huduma ya usafiri wa abiria wa ndani’daladala’kama ilivyo kwa mikoa mingine

Ukarabati njia panda

Uhakika wa wanafunzi waliopelekwa uhamishoni kurejea tena kwenye shule yao kwa miezi michache ijayo hauko wazi baada ya Manispaa ya Bukoba kusitisha ukarabati mdogo itakapofanyika tathimini ya kina.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Limbe Moris anasema wanafunzi hao wataendelea na masomo katika shule walizopelekwa na hakuna ukarabati mdogo utakaofanyika hadi mapendekezo ya wataalamu yatakapotolewa.

‘’Wanafunzi wataendelea na mafunzo yao kwenye shule walizpelekwa baada ya hatua za dharula kuchuliwa suala hili limeishachukulwa na Serikali kuu kwa ajili ya kutafanyika tahmini ya kina hata ukarabati mdogo tumeacha’’anasema Moris

Kuhusu changamoto ya umbali wa kusafiri kwa wanafunzi Mkurugenzi huyo anasema hata kabla ya shule hiyo kufungwa wanafunzi walikuwa wanasoma kutwa na kurejea nyumbani na wataendelea kufanya hivyo hata walipopelekwa.

Anasema kuwa wamefanya mazungumzo na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri(Sumatra)ili kuwa na magari ya abiria yanayokwenda Ihungo kila siku ili kupunguza adha ya usafiri kwa wanafunzi na walimu.

Katibu wa Wizara ya Elimu

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Dk Leonard Akwilapo anasema Bukoba ni miongoni mwa sekondari kongwe hapa nchini na Wizara itatuma timu ya wataalamu kwa ajili ya kufanya tathimini ya kina kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa.

Anasema taarifa ya wataalamu itaonyesha ni kitu gani kinatakiwa kufanyika katika shule hiyo kama ni kufanya ukarabati wa majengo yake au kuanza ujenzi upya baada ya msingi kutokuwa na uwezo wa kubeba majengo hayo tena.

Anaridhika na hatua za dharura zilizochukuliwa ili kukabiliana na tatizo hilo akisema shule walizopelekwa zina miundombinu ya kuweza kuhimili idadi hiyo na kuwa huenda maafa yangekuwa makubwa siku ya tukio kama wanafunzi wangekuwa darasani.

Chanzo: mwananchi.co.tz