WATU tisa wamefariki dunia na wengine 51 kuolewa, baada ya boti ya MV. Nzaimana kuzama katika Ziwa Tanganyika.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kigoma, Martin Otieno, alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya alfajiri wakati boti hiyo ikiwa safarini kutoka eneo la Sibwesa wilayani Uvinza kuelekea Ikola, mkoani Katavi.
Kamanda Otieno alieleza kuwa taarifa za awali zinaeleza boti hiyo ilikuwa imebeba abiria wapatao 60 wakiwa na mizigo yao midogo midogo na bidhaa zingine.
Kwa mujibu wa Kamanda Otieno, wakiwa wanaendelea na safari boti hiyo ilipigwa na dhoruba kisha kuzama.
“Taarifa tulizonazo hadi sasa hivi kuna watu tisa wameopolewa wakiwa wamekufa, kati yao wanawake saba na wanaume wawili,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda Otieno alisema asingeweza kueleza kwa undani kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa alikuwa njiani kuelekea eneo la tukio kuona uhalisia.
Alisema kuwa baada ya kufika na kushuhudia, atauelezea zaidi undani wa tukio lilivyokuwa .
MGANGA MKUU WA WILAYA
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dk. Ruben Mwakilima, aliieleza Nipashe kuwa walipokea majeruhi watatu wa ajali hiyo kwa ajili ya matibabu katika zahanati ya Sibwesa majira ya asubuhi, huku wengine wakiendelea na ratiba zingine kutokana na kutopata athari zozote.
Dk. Mwakilima alisema hadi kufikia jioni, walikuwa wamepokea miili minane kutoka eneo la tukio.