Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi trafiki awaonya bodaboda

61476cb858379c3853d5d07931e62e03 Bosi trafiki awaonya bodaboda

Thu, 17 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Solomon Mwangamilo amewaonya waendesha pikipiki (bodaboda) wanaochakachua vyombo hivyo ili vitoe mlio mithili ya bomu.

Amewataka waache mara moja, la sivyo watakamatwa katika operesheni maalumu itakayofanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Alisema hayo katika kikao kazi kilichozungumzia changamoto za usafiri wa bajaji na pikipiki kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani.

Solomon alisema milio hiyo imekuwa kero na inaleta mshtuko kwa wasiopenda kelele. Wakati mwingine milio hiyo imesababisha vifo kwa watu wenye maradhi ya moyo.

Alisema vyombo hivyo vinatengenezwa viwandani vizuri, lakini madereva hao wanazichakachua na kuanza kusumbua mitaani na barabarani kwa kupiga ovyo milio hiyo.

"Kweli hii imekuwa kero kubwa maana kama kuna mtu mwenye ugonjwa wa moyo au hospitalini, inaleta shida, hata mimi mwenyewe juzi kidogo nikimbie, nilikuwa mahali nikasikia mlio kama bomu kuangalia pikipiki imeshakimbia," alisema.

Alisema kutokana na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa mengi, jeshi hilo limejipanga kuendesha operesheni ya kuzikagua pikipiki hizo zilizochakachuliwa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Alisema wameanza kutoa elimu kwenye vijiwe vya bajaji na pikipiki ili kupunguza ajali barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na madereva wa vyombo hivyo kutojua sheria za usalama barabarani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salum Hamduni alisema ni vyema kila mmoja wao, atii sheria za usalama barabarani, ili kutolazimisha jeshi hilo kutumia nguvu kwao.

"Tiini sheria kwani sipendi kutumia nguvu sana kwenu, naomba kila mmoja atii na kuzifuata sheria za barabarani, ili mkoa wetu tupunguze ajali," alisema.

Alisema matukio ya ajali ni mengi; na mengi yanasababishwa na madereva wa bajaji na pikipiki.

"Kutoka Januari hadi Novemba mwaka huu jumla ya ajali 647 zilitokea na katika ajali hizo watu 63 walipoteza maisha, majeruhi ni 60 na 99 walipata majeraha madogo. Lakini pia kuna ajali 924 ndogondogo zilitokea zilizosababishwa na bajaji na pikipiki,"alieleza.

Chanzo: habarileo.co.tz