Baadhi ya wafanyabishara katika eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam wamelalamikia hatua ya kuvunjwa kwa fremu za maduka yao yanayomilikiwa na familia ya Marehemu ya Mzee Haule, wakisema imewaathiri pakubwa kibiashara.
Wakizungumza wafanyabishara hao wamedai kuwa kuathirika huko kunatokana na zoezi hilo kufanywa kwa kushitukiza wakati wakiendelea na biashara.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwenge, Kata ya Kijitonyama Jijini Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ramadhan Shelukindo, amesema licha ya wafanyabishara hao kupewa muda mrefu kuondoa bidhaa zao bado walikaidi kufanya hivyo na kwamba zoezi la kuvunja eneo hilo limesimamiwa vizuri kwa kuzingatia taratibu za kisheria.
Pamoja na mambo mengine, mwenyekiti huyo ameeleza kuwa fremu hizo zimevunjwa baada ya mahakama kutatua mgogoro wa wanafamilia ambao umedumu kwa miaka mitatu ili kila mmoja apate haki yake.