Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi ya Maji yavunjwa, Naibu Waziri amtumbua meneja

27db65d06f67fe6127e84c529479543d.jpeg Bodi ya Maji yavunjwa, Naibu Waziri amtumbua meneja

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Waziri wa Maji, Marypriscar Mahundi amevunja Bodi ya Maji ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rujewa wilayani Mbarali.

Aidha, Mahundi pia amemvua cheo Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji (Ruwasa) wilayani hapo, Job Mwakasala, baada ya kukuta miradi aliyoiita kichefuchefu.

Alifanya uamuzi huo baada ya kukerwa na maandalizi mabovu ya ziara wilayani humo sambamba na utekelezaji mbovu wa miradi ya maji kutokana na uzembe wa watendaji hali inayosababisha wananchi waendelee kuteseka kwa kukosa maji.

"Nimekerwa na miradi wilayani hapa… Hatuwezi kuendelea kuwa na watendaji wa namna hii... Lazima kufanyika mabadiliko kuanzia kwa meneja wa Ruwasa na ikiwezekana ‘staff’ wote waondolewe,” alisema Naibu Waziri.

Akaongeza: “Serikali inajitahidi kuboresha maisha ya wananchi, lakini watendaji wanakwamisha jitihada hizo sasa lazima wale wanaoleta jeuri, wakae kando tutafute wengine wanaoweza kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano."

Miongoni mwa miradi iliyomkera Naibu Waziri Mahundi ni ule wa Luduga-Mawindi ambao ni miaka saba sasa tangu uanze kutekelezwa,lakini haujakamilika huku mabomba yakiwa yametelekezwa katika Kijiji cha Kangaga, Kata ya Mawindi huku zaidi ya Sh bilioni 4.5 zikiwa zimetumika.

Kukamilika kwa mradi huo kungenufaisha wakazi katika vijiji vya Kangaga, Mkandami, Matemela, Ipwani, Itipingi na Manienga. Hivi sasa wakazi wa vijiji hivyo wanalazimika kutumia vyanzo vya maji vinavyotumiwa na mifugo.

Hadi kukamilika, mradi huo unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 12.3.

Kwa mujibu wa uchunguzi, kingine kilichomkera Mahundi katika mradi huo, ni uwepo wa fedha zilizotolewa na serikali tangu Agosti mwaka jana na zimeendelea kukaa benki huku Meneja wa Ruwasa wilayani humo akisingizia uwepo wa mvua nyingi kukwamisha ulazaji wa mabomba.

Mahundi aliikataa hoja hiyo akisema hatua ya uchimbaji mitaro na kulaza mabomba haiwezi kuwa na utetezi wa kisingizio cha mvua nyingi kwa kuwa ndiyo kwanza zinaanza kunyesha wilayani humo na pia wakati fedha hizo zinatolewa, hakukuwa na mvua.

Mradi mwingine ni wa Uhamila katika Kata ya Rujewa unaodaiwa kutokuwa na tija kwa wananchi kwa kuwa umekuwa kama mapambo kwa kutotoa maji.

Diwani wa Kata ya Rujewa, Michael Makao, alisema awali mradi huo ulikuwa ukitoa maji kwa kusuasua na baadaye maji yakakata kabisa.

Maelezo hayo yaliyotofautiana na ya wataalamu akiwemo Meneja wa Mamlaka ya Maji ya Mji Mdogo wa Rujewa ambaye baada ya Naibu Waziri kumpigia simu, alisema maji yalitoka hata asubuhi na pia akasema, hakuwa kwenye ziara hiyo kwa sababu alikuwa safarini Musoma kumuuguza mama yake.

Mradi mwingine uliomkera Mhandisi Mahundi ni wa kisima uliopo katika Kata ya Magongole wilayani Mbarali.

Serikali ilitoa Sh milioni 70 ambazo zimeendelea kukaa benki huku kukiwa hakuna shughuli zinazoendelea licha ya uwepo wa kisima kilichochimbwa muda mrefu huku wananchi wakiendelea kuhangaika.

Kilichomkera zaidi Naibu Waziri ni wataalamu wa Ruwasa wilaya kumuandalia mradi mmoja wa maji kuutembelea ambao ni wa Luduga-Mawindi hatua ambayo ingeufanya msafara wa kiongozi huyo kumaliza kazi yake saa tano asubuhi jambo alilolikataa na kulazimika kujiongezea miradi mingine.

"Wakati nikitoa maamuzi ya watendaji kuondolewa nimefikiria pia sana kuhusu wajumbe wa bodi... Nimejiuliza hivi inakuwaje bodi ipo halafu uchafu kama huu unafanyika. Hatuwezi kuwa na wajumbe wa bodi wanaojiona ni sehemu ya menejimenti. Kuanzia leo naivunja bodi na itakapoundwa bodi nyingine asiwepo hata mjumbe mmoja wa sasa." alisema Naibu Waziri Mahundi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune alisema uhalisia ni kuwa upatikanaji wa maji ya bomba katika maeneo mengi wilayani humo hauendani na taarifa zinazotolewa na wataalamu wa Ruwasa kwa viongozi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbarali, Hashim Mwalyawa alisema jambo la kusikitisha ni pale miradi inapoonekana kutokamilika na kusababisha kuwepo kwa miradi sugu huku sababu hasa za kushindwa kukamilika zikiwa zinatokana na uzembe wa wataalamu licha ya serikali kutoa fedha.

Chanzo: habarileo.co.tz