Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi shule za Alliance kujadili wizi wa mitihani

20681 Pic+mtandao TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Bodi ya wakurugenzi wa shule za msingi Alliance na New Alliance za jijini hapa imesema itaitisha kikao kujadili kutajwa kwa shule hizo katika udanganyifu na kuvujisha mtihani wa Taifa wa darasa la saba uliofanyika Septemba 5 na 6.

Mbali na shule hizo, nyingine zilizokumbwa na rungu hilo ni  shule zote za msingi Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, shule ya Kondoa Integrity iliyopo Dodoma pia; Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy za Dar es Salaam na Kisiwani ya Mwanza.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumatano Oktoba 3, 2018  mkurugenzi mtendaji wa shule za Alliance, James Bwire amesema shule hizo zina wakurugenzi wengi, yeye hawezi kuzungumza lolote bila kufanyika kwa vikao.

Licha ya kutotaja siku kitakapofanyika kikao hicho, amesema kitafanyika mapema zaidi na atatoa taarifa kwa vyombo vya habari

"Ni kweli mimi ndiyo mkurugenzi mtendaji lakini hii ni taasisi ambayo ina viongozi wengi na ili kuchukua uamuzi wowote ni lazima tukae wote,” amesema.

MCL Digital imefika katika shule hizo leo lakini imezuiwa kuingia katika majengo ya shule, huku baadhi ya wazazi waliokuwepo eneo hilo wakisema ni muhimu shule kuweka utaratibu mzuri wa wanafunzi kurudia mtihani huo kama ilivyopangwa na Baraza la Mitihani (Necta).

Mmoja kati ya mzazi mwenye mtoto katika shule hiyo, Elikana Mwita amesema, "Kiukweli hii taarifa sijaipenda, unakuta umewekeza kwa wanao ili na wao waje kukusaidia mbeleni lakini sasa yakianza haya nashindwa kwa kweli.”

Chanzo: mwananchi.co.tz