Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi chama cha Ushirika Milambo yavunjwa

4444732151f6604ee08500dd0002a957 Bodi chama cha Ushirika Milambo yavunjwa

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BODI ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo Ltd mkoani Tabora, imevunjwa kwa kushindwa kushughulikia kikamilifu suala la wizi wa pembejeo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 55 huku ikiamuriwa kuzirejesha pembejeo hizo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari ilisema, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk Benson Ndiege alivunja bodi hiyo juzi kwenye kikao kilichofanyika mjini Urambo ambacho kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa.

Ndiege baada ya kuvunja bodi hiyo aliwataka wajumbe wake kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili waliosababisha au kuhusika katika wizi huo wa pembejeo wajulikane na kuchukuliwa hatua.Vile vile alizuia wajumbe wa bodi iliyovunjwa kugombea uongozi wa bodi katika vyama vyao vya ushirika vya msingi na chama kikuu.

Pia aliagiza mtunza ghala kusimamishwa kazi au kuondolewa kazini kwa kufuata taratibu za utumishi zinavyoelekeza ikiwa ni pamoja na kumuagiza Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo, Leak Madele kuandaa taarifa ya kina kuhusu wizi huo.

Taarifa hiyo itahusu kuanzia kipindi cha maombi ya mbolea kutoka kampuni ya Petrobena, kusambazwa kwenye AMCOS, mikataba iliyotumika, pembejeo zilizopokelewa na utaratibu uliotumika.

Mkuu wa wilaya hiyo Angelina Kwingwa alisema kuwa baada ya kupewa taarifa ya wizi wa pembejeo uliotokea katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo alikwenda na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwenye ghala la chama hicho ulipotokea wizi na kufanya mahojiano na Wahusika.

Alisema taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuhusu wizi huo iliahidiwa kukabidhiwa kwa Mrajis mara baada ya kikao hicho.

Chanzo: habarileo.co.tz