Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodaboda yakatisha ndoto ya aliyefaulu daraja la kwanza

91498 Bodaboda+pic Bodaboda yakatisha ndoto ya aliyefaulu daraja la kwanza

Mon, 13 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Ni majonzi na simanzi kwa jumuiya ya shule. Taarifa za kifo cha Honest Mulokozi zimeibua taharuki kwa wanafunzi wetu na kufanya uongozi kulazimika kufanya kazi ya ziada ya kuwashauri na kuwatuliza.”

Hiyo ni kauli ya Padri Marianus Rutagwerera, mkuu wa shule ya Seminari ya Rubya mkoani Kagera alipozungumzia kifo cha mwanafunzi Honest aliyetakiwa kuingia kidato cha tatu shuleni hapo mwaka huu baada ya kupata ufaulu wa daraja la kwanza katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

“Kifo hiki kimekatisha ndoto ya Honest ya kuwa padri. Wazazi wake walimkabidhi (kwetu) tumfundishe na kumlea ili amtumikie Mungu; na yeye alikuwa akipenda kuwa padri, lakini ndiyo hivyo ndoto yake imekatishwa na kifo,” alisema mkuu huyo wa shule.

Akisimulia jinsi taarifa za kifo hicho kilivyopokelewa shuleni hapo, Padri Rutagwerera alisema, “ni mshtuko na majonzi hadi nashindwa kusema.”

Katika mazungumzo yake na Mwananchi kwa simu jana, kiongozi huyo wa kiroho alisema taarifa za kifo hicho kinachodaiwa kusababishwa na ajali ya pikipiki (bodaboda) kiligeuza eneo la shule kuwa la msiba likigubikwa na vilio kutoka kwa wanafunzi na watu wengine.

“Tulilazimika kuwatumia walimu na watumishi wengine wenye taaluma ya ushauri na malezi kuwatuliza wanafunzi wetu ambao kila mmoja alikuwa akilia kivyake. Namshukuru Mungu utulivu umerejea,” alisema.

Alisema ingawa Honest alikuwa hajachagua fani kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa aingie kidato cha tatu ambako angechagua achukue masomo. Padre Rutagwerera anaongeza uwezo wake darasani ulikuwa mkubwa kwa sababu alikuwa anamudu masomo yote.

Alisema wakati wa uhai wake, Honest alikuwa akisema angependa kuwa kwenye orodha ya watu walioiletea sifa seminari ya Rubya kwa matokeo mazuri.

Miongoni mwa watu maarufu nchini waliosoma kwenye Seminari ya Rubya iliyoanzishwa mwaka 1904 ni majaji, maaskofu, wanasheria na wanasiasa.

Dada azungumza

Piece Juventus, ambaye ni dada wa marehemu, Honest aliiambia Mwananchi kuwa familia imeshtushwa na kifo hicho cha ghafla.

“Honest alikuwa na ndoto nyingi kimasomo lakini maisha yake yamekatishwa na kifo hiki cha ajali ya pikipiki,” alisema Piece.

Honest alifariki baada ya kupata ajali katika eneo la Kyaka wilayani Misenyi wanakoishi wakati akielekea kijiji cha Bushangalo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera na mazishi yake yanatarajiwa kufanyika leo.

Matokeo ya mtihani

“Marehemu Honest aliyefariki katika ajali ya pikipiki alikuwa miongoni mwa wanafunzi 47 waliofanya mitihani ya kidato cha pili shuleni kwetu na wote wakafaulu daraja la kwanza,” alisema Padre Rutagwerera na kuongeza, “Yote ni mapenzi ya Mungu. Lakini ni pigo na pengo kwetu sote.”

Tahadhari wakati wa mazishi

Kutokana na hali iliyojitokeza baada ya taarifa za kifo kuwafikia wanafunzi, uongozi wa Rubya Seminari umeamua kuchukua tahadhari kukabiliana na hali itakayojitokeza wakati wa mazishi ya mwanafunzi huyo yanayotarajiwa kufanyika wilayani Karagwe leo.

“Tunahofia hali ya simanzi na majonzi itawarejea wanafunzi wenzake tutakaokwenda nao kwenye mazishi mara watakaposhuhudia mwili wa mwenzao, tumewaandaa watu wa kuwashauri, kuwasaidia na kuwapa huduma ya kwanza itakapolazimu,” alisema Padri Rutagwerera.

Chanzo: mwananchi.co.tz