Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodaboda wapewa somo hili usalama barabarani

E8c5c153a51dc7f16c5f4988b85c3917.jpeg Bodaboda wapewa somo hili usalama barabarani

Mon, 27 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amewataka madereva wa pikipiki maarufu kwa jina bodaboda wilayani humo wazingatie sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kufunga vioo vya pembeni na kuvaa kofia ngumu.

Mtatiro alitoa agizo hilo alipozungumza na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) mjini Tunduru.

Alisema matukio ya ajali za pikipiki yameongezeka na kila wanapofuatilia wanabaini baadhi ya ajali hizo zinatokana na uzembe na madereva kutozingatia sheria.

Mtatiro aliliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo lianze operesheni kukamata pikipiki zisizokuwa na vioo vya pembeni na pia kuwakamata na kuwashitaki mahakamani wanaoendesha vyombo hivyo bila kuvaa kofia ngumu.

Alisema katika operesheni hiyo watakamata watu wote wasiotaka kutii sheria bila shuruti hata wakiwa viongozi.

“Ndugu zangu, nimelazimika kusema haya kwa sababu nyinyi ni viongozi na baadhi yenu mnaendesha na kumiliki pikipiki, tukikukamata utalala ndani na kesho tunakufikisha mahakamani. Hatutaki kusikia kila siku tunapoteza watu kutokana na ujinga,” alisema Mtatiro.

Aliomba viongozi hao wasaidie kufikisha elimu ya usalama barabarani kwa wanachama wa vyama msingi vya ushiriki katika maeneo yao.

Mtatiro alisema wataanza kusajili vijiwe (vituo) vya bodaboda na madereva wa pikipiki watapewa sare ili kuwatambulisha zikiwa na jina la kijiwe husika na namba ili iwe rahisi kuwatambua.

Alihimiza wananchi katika wilaya hiyo waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa kupata chanjo katika vituo vilivyotengwa na serikali.

Alisema chanjo hiyo ni salama na hakuna madhara anayopata anayechanjwa hivyo wananchi wapuuze kauli za upotoshaji kuwa chanjo zina madhara.

Katika hatua nyingine, Mtatiro alisema ifikapo Desemba 30 mwaka 2022 vijiji vyote katika wilaya hiyo vitakuwa vimeunganishwa na nishati ya umeme, hivyo wananchi wajiandae kuingiza umeme kwenye nyumba zao.

Mtatiro aliwataka viongozi wa serikali za vijiji na kata watoe ushirikiano kwa wakandarasi na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya umeme katika maeneo yao.

Chanzo: www.habarileo.co.tz