Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodaboda walivyomdhibiti mtu aliyemjeruhi mpenzi kwa risasi

97492 Pic+bodaboda Bodaboda walivyomdhibiti mtu aliyemjeruhi mpenzi kwa risasi

Sat, 29 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Mara nyingi imezoeleka kuwaona waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda wakimkimbiza dereva wa gari aliyemgongo mwenzao na kujaribu kukimbia.

Kumbe tabia na hulka ya madereva bodaboda ya kuwadhibiti na kufanikisha kukamatwa kwa wanaofanya makosa na kujaribu kukimbia mikono ya sheria si penye maslahi yao pekee, bali ni kwa makundi mengine ndani ya jamii.

Ukweli huu umejidhihirisha mjini Geita juzi baada ya waendesha bodaboda kumkimbiza na kufanikisha kumkamata mfanyabiashara wa Mwanza, Salum Othuman (44) aliyejaribu kukimbia akitumia gari binafsi baada ya kumjeruhi mpenzi wake kwa kumpiga risasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo aliiambia Mwananchi jana kuwa mfanyabiashara huyo anadaiwa kumjeruhi kwa kumpiga risasi mguuni mpenzi wake, Happiness Israel (32) katika tukio lililotokea saa 4:00 asubuhi Februari 26, 2020 wakiwa chumbani katika Hoteli ya Kilimanjaro mjini Geita.

“Baada ya kumjeruhi kwa risasi, mfanyabiashara huyo alimpakia mpenzi wake kwenye gari lake kwa nia ya kuondoka hotelini hapo na alipofika getini alimjeruhi mlinzi anayeitwa John Maftari kwa kugonga geti na kumburuza, alipojaribu kumzuia kutoka,” alisema Kamanda Mwabulambo

Kutokana na mlio wa risasi, kutishia wafanyakazi kwa bastola, kuvunja geti na kumjeruhiwa mlinzi, waendesha bodaboda waliokuwepo jirani walioshuhudia tukio hilo walianza kumkimbiza mtuhumiwa huyo na kufanikisha kutiwa kwake mbaroni.

Pia Soma

Advertisement
Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Paulo Lyimo alisema mtuhumiwa ambaye ni mteja wao wa mara kwa mara hotelini hapo, alionekana akiwa amembeba mpenzi wake aliyekuwa akivuja damu mguuni akitoka naye chumbani.

“Wafanyakazi walipojaribu kumzuia kuondoka aliwatishia kwa bastola na kulazimisha kuondoka kwa kuparamia geti na kumjeruhi mlinzi. Waendesha bodaboda waliokuwepo jirani kumfukuzia hadi alipotiwa mbaroni,” alisimulia Lyimo.

Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita, Dk Shaban Masawe alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Happiness amevunjika mfupa wa paja huku John akiwa na michubuko maeneo mbalimbali ya mwili.

“Majeruhi ambaye ni Happiness alitibiwa kwa dharura katika hospitali ya mkoa Geita na kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi huku yule mlinzi akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Geita,” alisema Dk Shaaban.

Chanzo: mwananchi.co.tz