Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodaboda kupambana wanaoendekeza ukatili

Ukatili Bodaboda kupambana wanaoendekeza ukatili

Wed, 3 Nov 2021 Chanzo: ippmedia.com

Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na vijana wanaoishi katika maeneo hatarishi kata ya Mabogini, Moshi Vijijini wameapa kupambana usiku na mchana dhidi ya watu ambao wanaendeleza vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ukatili wa ngono.

Vijana 40 walioungana kufanya kazi ya kupaza sauti zao kupinga ukatili wa kijinsia kutoka vijiji vya Mserekia, Mvuleni, Mabogini na Mtakuja, waliweka wazi dhamira yao hiyo juzi walipokuwa wakitoa elimu katika Soko la Chekereni, Kata ya Magogini.

Akizungumza wananchi waliokuwa katika soko hilo, Yusto Joachim, mkazi wa Kijiji cha Mtakuja, alisema katika pitapita zao walichokigundua ni kwamba wako wazazi wengi wana maumivu na wanaona haya kuyasema au kupaza sauti zao.

Alisema vitendo hivyo vimekuwa havitolewi taarifa kwa kuwa wanaofanya matukio hayo ni watu wa karibu wakiwamo majirani, marafiki na ndugu.

“Kazi hii tutaifanya iwe mvua, iwe jua. Sasa ombi leti ni vyema watendaji wa vijiji au wenyeviti wetu wa serikali za vijiji wawe tayari kwenye vikundi kule vijijini kututambulisha kwenye mkutano wa hadhara wa kijiji,” alisema.

Bernard Saitore, alisema licha ya kufurahia utoaji wa elimu hiyo kwa jamii, amekutana na vikwazo vingi, hasa suala la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, ambalo watu wanaishi nalo na hawataki kusema hadharani, wakiogopa watachomewa nyumba, kuambulia vipigo na kudhalilika.

Alisema kikwazo kingine alichobaini ni jamii kutojua pa kuwasilisha taarifa ili kupata msaada.

Songelael Elia, mkazi wa Kijiji cha Mserekia, alisema wananchi wamewapokea vizuri na wanatamani kufanya nao kazi na walitamani wawape wao taarifa kwa kuwa baadhi ya viongozi wa vijiji, kata na hata baadhi ya askari polisi wanatumika wakati mwingine kuficha tatizo.

Kabla ya vijana hao kuanza kutoa elimu hiyo sokoni Chekereni, Mratibu wa Mradi wa Paza Sauti, Tokomeza Ukatili, unaotekelezwa na Shirika la TUSONGE CDO kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society (FCS), Consolatha Kinabo, alisema:

“Katika hatua mojawapo ya mradi kama mpango mkakati, tumeona kuna uhitaji wa sisi kuwa na vijana ndani ya jamii ya Kata ya Mabogini ili nao basi wabadilike.

"Wawe na mitazamo chanya ya kulinda, kutetea na kujiingiza katika uelimishaji wa haki za binadamu, hasa kupinga vitendo vya ukatili ndani ya jamii.

“Tumeshirikiana na uongozi wa vijiji na kata pamoja na kamati za MTAKUWWA (Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto), kutafuta na kuwajengea uwezo vijana, ambao wanaweza kupigiwa mfano, haijalishi kama alikuwa na mienendo ambayo haipendezi, lakini tunajua kijana ana nguvu, ana uwezo wa kubadilika na kuwa na mchango ndani ya jamii yake.

“Vijana waliojengewa uwezo ni bodaboda, vijana wanaoishi katika maeneo hatarishi na vijana wanaohusiana na wanajamii.

"Tumewapatiwa elimu juu ya usawa wa kijinsia, nini maana ya ukatili, jinsia ni nini, mgawanyo wa majukumu ndani ya familia na mikinzano juu ya mitazamo hasi kuhusu mfumo dume ndani ya jamii.

"Ni kwa namna gani wanaweza kubadilisha mitizamo hiyo na wakawa na mawazo chanya na wakawa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kubadilika, kutetea na kulinda haki za wanawake ndani ya jamii yao.”

Vijana hao waliwezeshwa na Shirika la TUSONGE CDO nyenzo mbalimbali za kazi hiyo ikiwamo tisheti, viakisi mwanga pamoja na stika ili wazitumie kupaza sauti na kutokomeza ukatili ndani ya jamii.

Chanzo: ippmedia.com