Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biskuti, keki za kahawa na upanuzi soko la ndani

B869c624b8cacc87b3868be0d89706dd Biskuti, keki za kahawa na upanuzi soko la ndani

Tue, 1 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MLIPUKO wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababisha na virusi vya corona (Covid-19) ulioikumba dunia, umekuwa na athari nyingi katika biashara zinazotegemea soko la nje, ikiwamo kahawa.

Taarifa za sasa zinaonesha kwamba covid-19 imesababisha makampuni yaliyonunua kahawa kutoka katika vyama vya ushirika kushindwa kuisafirisha nje ya nchi kutokana na mataifa mbalimbali kufunga anga zao.

Kushindwa kusafirisha kahawa hiyo kwa wakati kumechelewesha malipo ya wakulima ambayo yanapitia moja kwa moja kwenye vyama vyao vya ushirika.

Soko kubwa la kahawa ya Tanzania ni nje ya nchi kupitia mnada ambao umekuwa ukifanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Kama ambavyo utalii umeathirika vibaya na corona kutokana na kutegemea zaidi watalii wanaotoka nje, ndivyo pia kahawa ya Tanzania inavyoathirika kutokana na utumiaji wa kinywaji hicho wa ndani ya nchi kuwa mdogo.

Inaelezwa kwamba unywaji wa kahawa nchini haujafikia hata asilimia 10.

Katika kipindi cha corona inayoendelea kutesa mataifa mbalimbali, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Kahawa nchini (TaCRI), Kanda ya Kagera, imekuwa ikijaribu kufanya utafiti kwa kushirikiana na wadau mbalimbali juu ya nini kifanyike ili kuhamasisha matumizi zaidi ya kahawa na hivyo kupanua soko la ndani.

Dhana iliyopo ni kwamba soko la ndani la kahawa likiongezeka, ajira kwa vijana ambao wanachukulia kilimo cha kahawa kama kilimo cha wazee zitaongezeka pia.

Mtafiti mwandamizi kutoka TaCRI- Kanda ya Kagera anasema mkoa huo unaolima takribani asilimia 45 ya kahawa yote inayolimwa nchini, Dk Nyabisi Ng’homa, anasema utafiti wao kuangalia namna ya kuboresha soko la ndani ulianza mwezi Machi baada ya covid-19 kulipuka duniani.

Anasema timu yao ilimaliza utafiti ulioshirikisha Bodi ya Kahawa, wadau na wadhamini mbalimbali mwishoni mwa Julai.

Anasema utafiti huo uliofanywa mkoani Kagera umeonesha kwamba soko la kahawa linaweza kupanuka maradufu hasa itakapotumika kwa wingi kama kiungo cha kuongeza ladha ya vyakula mbalimbali.

Kutokana na utafiti huo, hatua ya kuanza kuelimisha umma kuhusu matumizi zaidi ya kahawa katika vyakula ilianza kutolewa katika viwanja vya maonesho ya kilimo, maarufu Nanenane Agosti 1 mwaka huu.

Ng’homa anasema makumi kwa mamia ya watu waliohudhuria maonesho ya Nanenane yaliyofanyika katika Manispaa ya Bukoba, waliweza pia kuonja vyakula mbalimbali vilivyotiwa ladha ya kahawa.

Ulikuwa ni wakati mzuri kwa wapishi mbalimbali wa keki na vyakula vya kwenye sherehe mbalimbali kutumia fursa hiyo kujifunza namna ambavyo kahawa inavyoweza kuchanganywa kwenye vyakula ili kuvutia walaji.

Wengi walioonja vyakula vilivyotiwa kahawa walijikuta wakitaka kujifunza zaidi namna ya kutengeneza mchanganyiko wa kahawa na vyakula vingine.

“Aliyeonja kwa mara ya kwanza leo, kesho yake anakuja na kalamu na karatasi kwa ajili ya kuchukua maelezo ili akajaribu kujitengenezea chakula kilichotiwa kahawa nyumbani,” anasema Mtafiti huyo.

Ng’homa anataja baadhi ya vyakula hivyo mbali na keki kuwa ni pamoja na biskuti, pipi, ice cream na mikate.

Mamia ya wakazi wa mkoa wa Kagera walieleza kuvutiwa na ladha ya kahawa inapoongezwa kwenye vyakula na pia walielezea kufurahia mafunzo kutoka kwa wataalamu wa TaCRI.

Gasper Mutembei akiwa na mkewe, wanasema wanatazamia kuboresha mgahawa wao wa familia kwa kuboresha vitafunwa mbalimbali kwa kuongeza kahawa kwenye mchanganyiko.

Mtafiti huyo mwandamizi anasema ni asilimia saba pekee ya Watanzania wanaotumia kahawa kama kinywaji hivyo uwepo wa vyakula vilivyoongezewa ladha ya kahawa vitaongeza watumiaji wa kahawa kwa asilimia 15 ifikapo 2023.

“Lengo ni kufikia asilimia 50 ya watanzania wote wanaotumia kahawa.

Tukifikia huko hakutakuwepo na hali ya kulialia juu ya soko kwa kuwa soko la ndani litakuwa limepanuka na hivyo kahawa nyingi itauzwa ndani kwa bei nzuri na kuongezewa thamani kwa ajili ya kuchanganya katika vyakula mbalimbali,” anasema.

“Katika kipindi cha corona, sikuwa ninapata usingizi mzuri nikijaribu kuwaza ni kwa njia gani tunaweza kuvisaidia vyama vya ushirika kuuza kahawa ya mkulima. Niliwatembelea wataalamu kujua kama kahawa ina madhara kama ikitumika kwenye kunogesha vyakula vingine ikaonekana hakuna tatizo,” anasema.

Anasema nchi ya Ethiopia imekuwa ikitumia kahawa yake kwa zaidi ya asilimia 50 kwa soko la ndani na kuuza nje kidogo, hivyo ni wakati wa Watanzania kubadilika na kupenda kutumia kahawa yao kama kinywaji na kama kiungo cha vyakula vingine.

Ofisa ubora wa bodi ya kahawa mkoani Kagera, Jimmy Mchao, anasema alishiriki katika zoezi la kuangalia namna kahawa inavyoweza kutumiwa kama kiungo na kuhamasisha unywaji zaidi wa kahawa, hatua anayosema ni muhimu sana.

Anasema ni wakati sasa vijana wanaofanya kazi katika viwanda vya kuzalisha mikate na keki kuoka keki zenye ladha ya kahawa huku wakitoa ushawishi kwa wateja ili kupenda kahawa inayozalishwa ndani.

Anasema Bodi ya Kahawa imebariki moja kwa moja matumizi ya kahawa kama kiungo katika vyakula vingine na itahakikisha matumizi haya yanaenea Tanzania nzima.

Anasema hamasa inaendelea kutolewa kwa kuwatembelea wapishi wakubwa ili kuwafundisha namna ya kutengeneza vyakula vyenye ladha ya kahawa sambamba na kupokea maoni ya watumiaji wa vyakula hivyo.

Café Africa, shirika lisilo la kiserikali linalotoa huduma za ugani juu ya uzalishaji kahawa ni moja ya taasisi zilizoshiriki maonesho ya Nanenane kupitia banda la TACRI.

Shirika hilo limeahidi pia kusaidiana na TaCRI katika kutoa elimu ya kutengeneza vyakula vyenye ladha ya kahawa.

Mratibu wa shirika hilo, Daniel Mwakalinga, anasema licha ya kuboresha kilimo cha kahawa lakini pia shirika hilo limeanza kuelimisha jamii juu ya matumizi ya kahawa kama kiungo kwenye vyakula sambamba na kuhamasisha wananchi kupenda kinywaji cha kahawa.

Anasema shirika hilo linaendelea kutoka mafunzo ya ugani katika wilaya za Kyerwa, Karagwe, Missenyi, Muleba na Bukoba vijijini na mjini na kwamba kila wilaya kuna vijana watano wanaojishughulisha na kilimo cha kahawa ambao watasaidiwa kufungua vibanda vya kahawa ili wananchi wajipatie kahawa kwa matumizi ya nyumbani kwa urahisi.

Anahimiza Watanzania kupenda kunywa kahawa ya Tanzania, hatua itakayosaidia kuboresha soko la kahawa nchini.

Ikiwa ni siku kadhaa tangu kumalizika kwa maonesho ya Nanenane, mwandishi wa makala haya alitembelea kiwanda cha kuoka mikate, keki na kuandaa vitafunwa mbalimbali cha Rutha Bakery kuona kilivyonufaika na mafunzo ya kutumia kahawa kama kiungo cha bidhaa zao.

Mwandishi alizingatia kwamba kiwanda hicho kilimtuma mmoja wa wafanyakazi wake wakati wa maonesho hayo kupata mafunzo ya matumizi ya kahawa kwenye vyakula.

Meneja wa kiwanda hicho, Rutha Ishengoma, anasema wamenufaika sana na hatua hiyo kwani tangu maonesho hayo yamalizike kumekuwa na ongezeko la wateja wanaotaka keki na vitafunwa mbalimbali vilivyotiwa ladha ya kahawa.

Anasema vitafunwa vilivyoongezewa kahawa vimekuwa vikipendwa kila kikicha na hasa wakati wa sherehe mbalimbali na harusi.

Meneja Masoko wa kiwanda cha kukoboa na kusaga kahawa ya unga Frank Maulid, anasema mara nyingi wakazi wa Bukoba wamekuwa wakichukua kahawa na kuchemshwa kwa ajili ya kuuza kwenye vijiwe vya kahawa na kwamba wateja wao wakubwa huwa ni wazee.

Lakini anasema, wiki chache baada ya kumalizika kwa maonesho ya Nanenane, kumekuwa na ongezeko la wateja wanaochukua kahawa inayotengenezwa kwa ajili ya kuwekwa kwenye chai moja kwa moja mezani (instant).

“Hii mara nyingi ilikuwa ni kwa ajili ya soko la nje. Wateja wa ndani walikuwa wachache sana lakini sasa wanaongezeka,” anasema.

Anapongeza hatua ya TACRI ya kupanua wigo wa matumizi ya kahawa na kutabiri kwamba huenda wakaleta mabadiliko makubwa katika soko la kahawa la ndani.

Wakati anafungua maonesho ya Nanenane na kuonja vyakula vilivyotiwa ladha ya kahawa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti alisema anaunga mkono juhudi za TaCRI katika kupanua soko la ndani la kahawa.

“Kutokana na janga la corona kuna wakulima ambao hawajalipwa baada ya soko la nje kuwa gumu lakini kama kahawa ingenunuliwa kwa wingi ndani, wakulima wangelipwa fedha zao kama kawaida. Ninawapongeza TaCRI kwa kuja na ubunifu huu na mimi nitaunga mkono ubunifu huu ili kuhakikisha soko la kahawa la ndani linaimarika,” alisema Gaguti.

Chanzo: habarileo.co.tz