Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Binti aliza watu

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Binti wa miaka 16 amewaliza watu ukumbini akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Anna-Rose Nyamubi baada ya kutoa ushuhuda jinsi alivyokatishwa ndoto yake ya elimu kwa kukataa kukeketwa.

Binti huyo ambaye sasa angekuwa kidato cha tatu, alishindwa kuendelea na masomo baada ya mama mzazi na bibi yake kumlazimisha kukeketwa na alipokataa alifukuzwa nyumbani na kuacha shule.

Alitoa ushuhuda juu ya ukatili wa kijinsia katika ufunguzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwenye ukumbi wa uwekezaji mjini hapa jana, mkutano ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids).

Alisema mama yake aliyeolewa na mwanamke mwenzie maarufu ‘nyumba ntobhu’ alimtaka akeketwe mwaka 2014 akiwa darasa la sita lakini alikataa na kutorokea Musoma kwa bibi yake mzaa mama akitokea kijijini kwao Ryamisanga, Butiama.

Alisema baada ya msimu wa ukeketaji kuisha, alirudi tena kijijini kwao na kuendelea na masomo kwa vile mwaka huo haukuwa msimu wa ukeketaji.

Akisimulia mkasa huo, binti huyo (jina linahifadhiwa) alisema alifanikiwa kumaliza elimu ya msingi na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Ryamisanga lakini mama yake akishirikiana na bibi aliyemuoa mama yake walikataa kumpeleka shule huku wakimtaka ajiandae kukeketwa kwa vile mwaka huo ulikuwa ni msimu wa ukeketaji.

“Niliwaambia Serikali imetoa elimu bure hivyo waniache nikasome, lakini walikataa wakaniambia kama nataka kusoma nitoke nyumbani nimtafute ndugu atakayekubali kunisomesha,” alisema binti huyo huku akiwa analia hali iliyosababisha washiriki nao kutoa machozi.



Chanzo: mwananchi.co.tz