Esha Salim mkazi wa Kijiji cha Muungano, Kata ya Kilomba, Halmashauri ya Mji Nanyamba amesikitishwa na kitendo cha binti ake kujinyonga kwa kutumia mtandio baada ya kuzuia kwenda kuangalia video kwenye mabanda majira ya usiku ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Kilomba.
Akizungumza na Mwananchi kijijini hapo, amesema kuwa siku ya tukio binti huyo aliamka mapema na kumsindikiza shambani, lakini baadaye alichukua baiskeli na kurejea nyumbani.
"Aliniacha akachukua baiskeli akarudi nyumbani. Muda wangu wa kurudi ulipofika nilichukua kuni kisha nikarudi nyumbani ambapo nilimkuta amekaa chini ya mwembe, baada ya salamu akachukua kuni na kupika chakula. Alipomaliza tulikula watatu yaani mimi marehemu enzi za uhai wake na mwanangu mmoja wa kiume," amesimulia.
"Baada ya kumaliza kula, kaka ake akamwambia kwa lengo la kumuonya kwamba binti aache kwenda kwenye video usiku kwa kuwa mazingira siyo salama na amekuwa akirudi usiku sana wakati anasoma. Hivyo inaweza kuathiri masomo yake kwakuwa alikuwa anakwenda saa mbili na kurudi saa saba usiku jambo ambalo binti hakufurahishwa nalo," amesema.
"Alikuwa na kawaida yaani tukiwa tunakula saa mbili usiku tukimaliza tu, anaondoka kwenye video mpaka usiku sana ndio alikuwa akirudi…
“Siku hiyo niliwaacha nikaenda kuongea kwa jirani, narudi ndani nikaingia jikoni ili nitoe vyombo nikaoshe, nikamkuta mwanangu ananing'inia, ameshajinyonga. Nilikimbia nikaita watu, halikuwa jambo rahisi kwangu," amesimulia.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara, ACP Isack Mushi amesema kuwa msichana mwenye umri wa miaka 13 alichukua hatua ya kujinyonga baada ya kuzuiwa na kaka yake kwenda kuangalia video usiku kwenye mabanda.
Msichana huyo ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilomba iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara amekutwa amefariki baada ya kujinyonga chumbani kwake kwa kutumia mtandio wake.
Uchunguzi wa daktari umebaini chanzo cha kifo ni kukosa hewa baada ya kubanwa na mtandio shingoni ambapo uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.