tbc_online's profile picture tbc_online Verified Bilioni 4 kujenga barabara Mbozi
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde amesema, bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini nchini (TARURA) katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeongezeka mara nne hadi kufikia shilingi bilioni 4 katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Amesema hayo leo Februari 14, 2023 alipopewa fursa ya kusalimia wananchi katika eneo la Mlowo wilayani Mbozi, akiwa katika ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mkoani humo.
“Wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani alikuta bajeti ya TARURA katika halmashauri ya Mbozi ilikuwa bilioni 1.7 lakini kwa sasa bajeti imepanda hadi kufikia bilioni 4 katika mwaka wa fedha 2022/2023.” amesema Silinde
Amesema kupitia mradi wa kujenga barabara katika maeneo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, barabara ya Ilolo - Ndolezi yenye urefu wa kilomita 11 inajengwa kwa kiwango cha lami katika wilaya ya Mbozi ambayo inaanza kutekelezwa hivi karibuni.
Aidha, Naibu Waziri Silinde ameeleza kuwa katika awamu ya pili ya mradi huo barabara kutoka Mlowo mpaka Isanza ya kilomita 10 itajengwa kwa kiwango cha lami ili kuwezesha wakulima kusafirisha mazao yao.