SERIKALI imetoa Sh Bilioni 15.69 kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji 105 ndani ya Mkoa wa Simiyu.
Akizungumza wakati wa kumtambulisha mkandarasi wa mradi huo meneja miradi mkoa kutoka Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Mhandisi Deusdedit Msanze amesema mradi huo ni wa miaka miwili.
Amesema mkataba wa mkandarasi Kampuni ya CCC Beign Industrial and Company Ltd unamtaka kumaliza mradi Septemba 2026, ambapo takribani wateja wa awali 3,465 wataunganishwa umeme hadi mradi utakapokamilika.
“Vitongoji 15 katika kila jimbo la Mkoa wa Simiyu vitaunganishiwa umeme,” amesema Msanze.
Meneja wa Tanesco Mkoa Alistidia Kashemeza amesema Simiyu ina vijiji 470 ambavyo vyote vimepatiwa umeme kupitia REA na kwamba mradi huo ukikamilika utasaidia uchumi wa mkoa kukua kwa haraka.
Amesema TANESCO kama wasimamizi wakuu wa mradi huo imejipanga kuhakikisha inasimamia mkandarasi huyo ili akamilishe mradi kwa wakati na kwa ufanisi kulingana na thamani ya fedha.