Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 24/- zawezesha wakazi 50,000 kupata maji safi

Water Bil 24/- zawezesha wakazi 50,000 kupata maji safi

Thu, 8 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZAIDI ya wakazi 50,000 wa Mji wa Isaka na Kata ya Kagongwa wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga wamenufaika na mradi wa maji safi na salama uliotekelezwa na serikali kwa asilimia 100 uliotumia Sh bilioni 24 hadi kukamilika kwake.

Mhandisi kutoka Mamlaka ya Usambazaji Maji kwa Miji ya Kahama na Shinyanga (Kashwasa), Sayi Kapera aliyasema hayo jana mbele ya Mhasibu Mkuu kutoka Wizara ya Maji, Ahadi Msangi alipotembelea mradi huo na tangi la maji eneo la Kitwana na mapitio ya maji eneo la Mbulu.

Kapera alisema zaidi ya watu 50,000 kutoka mji wa Isaka na Kagongwa wamenufaika na mradi wa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa matangi mawili yenye ujazo wa lita 800 kila moja.

“Kuna jumla ya vioski 16 vya kuchotea maji na Kagongwa viko vioski saba na matangi mawili yenye ujazo wa lita 800 na Isaka kuna vioski tisa na matangi matatu yenye ujazo wa lita 300 kila moja, hivyo kwa upande wa Isaka wananchi wanaofaidika na maji ni 16,119 na Kagongwa ni 35,010,” alisema.

Meneja ufundi kutoka Mamlaka ya Maji mjini Kahama (Kuwasa), Paul Luchanganya alisema zipo changamoto kwa wateja kupungua sababu ya umbali wa kuunganisha kwani zinahitajika kilomita 17 na Kuwasa haina fungu hilo, hivyo wameiomba wizara kuwapatia fedha ili kuwarahisishia wateja waweze kujiunga zaidi.

Hata hivyo, mhandisi Magigwe Marwa kutoka Kuwasa alisema matangi mawili moja lililopo eneo la Kitwana lenye ujazo wa lita 135,000 huku eneo la Gongwa lenye ujazo wa lita 680,000 yamekamilika na yamegharimu Sh bilioni 2.4.

Kaimu Meneja wa Ruwasa, Mkoa wa Shinyanga, Juliette Payovera alisema hadi kufikia Septemba mwaka huu hali ya upatikanaji wa maji ni asilimia 60.03 kwa vijijini na mjini ni asilimia 70, kwa ujumla mkoa mzima makadirio asilimia 96.1.

“Ikiwa Mamlaka ya Maji Shinyanga ( Shuwasa) upatikanaji wa maji ni asilimia 80.03 na Mamlaka ya Maji Kahama ( Kuwasa) upatikanaji wa maji ni asilimia 85 na Kashwasa amebaki kuwa msambazaji pekee katika mamlaka hizo mbili na tangu kuanzishwa kwa Ruwasa walianza kutekeleza miradi 12 na yote wamekamilisha,” alisema Payovera.

Mhasibu Mkuu kutoka Wizara ya Maji, Msangi alipotembelea miradi hiyo alisema wataalamu waendelee kuhamasisha wananchi ili waunganishwe kwenye mtandao wa kupata maji safi na salama. Alisema zaidi ya watu 50,000 ni wengi kwani awali mji wa Isaka na Kagongwa walikuwa wakipata maji watu chini ya asilimia 10.

Chanzo: habarileo.co.tz