Serikali imesaini mikataba miwili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi (km 160) pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti yenye jumla ya shilingi Bilioni 234.512 kwa lengo la kuwaondolea wananchi wa Mtwara kero ya usafiri na usafirishaji.
Tukio hilo limefanyika wilayani Newala mkoani humo ambapo limeshuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa na viongozi wengine wa mkoa, wabunge na wananchi ambapo pamoja na mambo mengine Prof. Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaboresha mtandao wa barabara na madaraja katika ukanda wa Kusini.
Akizungumza na wananchi wa mkoa huo wakati wa hafla hiyo, Prof. Mbarawaameeleza kuwa barabara hiyo itaboresha usafiri na usafirishaji wa malighafi za viwandani kama makaa ya mawe na saruji, mazao ya chakula na kilimo, mifugo, uvuvi, bidhaa za kibiashara na mazao ya misitu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara pamoja na mikoa jirani ya Lindi, Ruvuma na Pwani kwenda maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Prof. Mbarawa, amewaasa wananchi wa Mtwara kutoa ushirikiano kwa makandarasi waliopata kazi ya ujenzi wa barabara hiyo pamoja na kujiepusha na vitendo vya uhalifu katika miradi hiyo.
“Hakikisheni mnatoa ushirikiano kwa vijana mtakaopata kazi katika mradi huu, muache tabia ya wizi wa vifaa, mkifanya hivi mtasababisha miradi kukamilika kwa wakati”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa ameahidi kuendelea kuufungua mkoa wa Mtwara kwa kuunganisha mkoa wa Lindi na mikoa jirani kwa barabara za lami pamaoja na ujenzi wa reli na bandari.
“Nimepokea maombi ya barabara mbalimbali ikiwemo ya kuunganisha kwa lami barabara ya Newala-Mtama, Mtama-Tandahimba, Mtwara-Kilambo, Newala – Mbuyuni ambapo fedha zimetengwa na upembuzi yakinifu na usianifu wa kina unaendelea”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas, amesema utekelezaji wa mradi huo unaunganisha wilaya zote za mkoa huo na hivyo kutaimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii na kupunguza gharama za maisha kwa mwananchi mmoja mmoja.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta, amesema kuwa Mikataba hiyo imesainiwa kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), na Kampuni ya China Wu Yi Co. Ltd sehemu ya kutoka Mnivata-Mitesa (Km 100), kwa gharama ya Shilingi Bilioni 141.964 na Kampuni ya China Communications Construction Co. Ltd atakayejenga sehemu ya pili kutoka Mitesa-Masasi (km 60) pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti kwa gharama ya Shilingi Bilioni 92.548. Eng. Besta ameahidi kuwa Wakala utasimamia vyema wakandarasi hao kukamilisha barabara hiyo kwa viwango vya ubora.
Pia ameongeza kuwa mradi huo utakuwa na miradi ya nyongeza kwa jamii ambapo wakandarasi watajenga Zahanati, Stendi, Shule, Maghala ya kuhifadhia mazao, Magari ya Wagonjwa na ununuzi wa X-Ray.Ujenzi wa barabara ya Mtwara-Newala-Masasi (km 160) ni moja ya mkakatinwa Serikali wa kuboresha mtandao wa barabara hapa nchini na ni kiungo muhimu kwa barabara kuu ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba bay inayojulikana kama Ushoroba wa Mtwara (Mtwara corridor) ambayo inaunganisha na nchi jirani ya Msumbiji.