Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 2/- zahitajika ujenzi stendi Sumbawanga

F52d1a2990414286e6623b56210103ff Bil 2/- zahitajika ujenzi stendi Sumbawanga

Tue, 15 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Jacob Mtalitinya amesema ili ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ya mji huo ikamilike, zinahitajika zaidi ya Sh bilioni mbili.

Alisema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alipotembelea eneo la Katumba Azimio inakojengwa stendi hiyo ili kuona ujenzi ulipofikia.

Alisema fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo, tayari zimekwisha na chanzo pekee cha fedha kilichobaki kwa ajili ya kumlipa mkandarasi ni makusanyo ya ndani ya halmashauri na fedha kutoka serikali kuu.

"Tumekuwa tukishauriana na mkandarasi ili aweze kukamilisha jengo hili la abiria angalau kufunika hizo 'fisher board' ili muonekano wa jengo na huduma zinazoweza kuanza zianze kwa sababu ya mahitaji ni makubwa”, alisema Mtalitinya.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) Manispaa ya Sumbawanga, Suleiman Mziray alisema katika mkataba wa awali stendi hiyo ilitakiwa kujengwa na jengo la chini pekee kwa gharama ya Sh bilioni 5.4.

Lakini, kamati ya uchumi na fedha ya manispaa ilishauri lijengwe ghorofa hivyo gharama iliongezeka na kufikia Sh bilioni 5.9.

"Vilevile wakati wa utekelezaji wa mradi huu kulikuwa na kazi zinaonekana zinaongezeka na kusababisha mpaka mkataba tulionao sasa hivi kufikia shilingi bilioni 7.2. Kazi ilianza Aprili 24, 2019 na inategemewa kumalizika Septemba 20, mwaka huu na kwa ujumla ujenzi umekamilika kwa asilimia 92," alisema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Sumry Enterprises inayojenga stendi hiyo, Humud Sumry alisema jambo kubwa linalokwamisha ujenzi wa stendi hiyo ni upatikanaji wa fedha, kwa kuwa wanadai karibu Sh bilioni 2.

Wangabo alisema kilichobaki ili stendi hiyo ianze kazi ni asilimia nane tu na vitu vidogo ambavyo vinaweza kufanyiwa kazi. Alisema ofisi ya mkurugenzi inajitahidi kutatua changamoto ya fedha.

"Stendi ikianza kufanya kazi mtaendelea kuingiza mapato mtalipana tena polepole wakati mnafuatilia hela Hazina kuliko kukaa kimya kukiwa na mdororo. Lakini pia tunapokaa muda mrefu kuna vitu vinaweza kupotea halafu maumivu ya stendi kutofanya kazi yakawa makubwa zaidi," alisema.

Stendi hiyo ya mabasi itakuwa na jengo la abiria 400, kituo cha polisi, baa, vyumba 16 vya kulala wageni, sehemu ya mazoezi (gym), ofisi 24 za kukatia tiketi, vyoo vya kulipia, vyumba vya benki na ATM, vibanda vya mlinzi na maduka 100.

Chanzo: habarileo.co.tz