Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil. 1.2/- kupeleka maji Kahama Vijijini

30153 Pic+maji Bil. 1.2/- kupeleka maji Kahama Vijijini

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Kahama (KUWASA) imetenga kiasi cha Sh. bilioni 1.2, kwa ajili ya kutekeleza miradi minne ya maji kwa wananchi wa vijiji na kata zilizopo pembezoni mwa mji, ambazo hazina huduma ya majisafi na salama.

Fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani ya mamlaka hiyo na zilitengwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 kuanzia na miradi hiyo inatarajia kukamilika mwaka 2021 na kuhudumia zaidi ya kaya 15,080.

Akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa miradi hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Meneja ufundi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Luchanganya Paul, alisema lengo ni kuongeza mgandamizo wa maji na kusogeza huduma ya maji kwa wananchi.

Alitaja miradi hiyo na kiasi cha fedha kwa kila mradi kuwa ni Mwanva-Mbulu zaidi ya Sh. milioni 686, Mwendakulima Sh. milioni 47, Chapulwa Sh. milioni 445 na Mhungula Mlimani Sh. milioni 67.

Meneja wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Allen Mwara, alisema miradi hiyo inatekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani.

“Mradi wa Mwanva-Mbulu mwanzo walitakiwa kutekeleza kwa kiasi cha Sh. milioni 915, lakini wanatekeleza kwa Sh. milioni 686 na kuokoa kiasi cha Sh. milioni 229,” alifafanua.

Alisema kati ya kata 20 zilizopo Halmashauri ya Mji wa Kahama, kata 15 zimeshapata huduma ya majisafi na salama na kukamilika kwa mradi wa Ngogwa Kitwana ambao utahudumia zaidi ya kata tatu na itakuwa imefikia idadi ya kata 18 zenye huduma hiyo.

Kwa upande wake, DC Macha aliipongeza mamlaka hiyo kwa kutekeleza miradi minne kwa wakati mmoja na kuwataka kuhakikisha ifikapo mwaka wa fedha 2020/21 kata mbili zinapata huduma ya maji kama ilivyo kwenye kata zenye maji.

Aidha, alilipongeza Gereza la Kahama kuchimba na kutandaza mabomba ya maji kama moja ya kuendelea kupunguza deni la maji wanalodai kwenye gereza hilo la zaidi ya Sh. milioni 140.

Mkazi wa Mbulu, Paulina Mabula, alipongeza mamlaka hiyo kwa kuwafikishia huduma ya maji kwenye makazi yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live