Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bibi auawa Morogoro, mwili wake wafunikwa mawe nje ya nyumba yake

Mauaji Abc.jpeg Bibi auawa Morogoro, mwili wake wafunikwa mawe nje ya nyumba yake

Mon, 3 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bibi mwenye umri wa (75) mkazi wa Mtaa wa Bong’ola Manispaa ya Morogoro aliyefahamika kwa jina la Mwajuma Sadru, maarufu Bibi Mzungu amekutwa ameuwawa na watu wasiojulikana na mwili wake kufunikwa na mawe nyumbani kwake.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Oktoba 3, mtoto wa marehemu, John Dofriana amesema kuwa yeye alipata taarifa za kutoonekana kwa mama yao Oktoba 2, 2022 asubuhi akiwa jijini Dar es Salaam, hivyo alisafiri hadi mkoani Morgoro na kuanza kumtafuta.

Dofriana amesema usiku wa tarehe hiyo wakiendelea kumtafuta mama yao ndipo walikuta mwili wake ukiwa umefunikwa kwa mawe umbali wa mita 50 kutoka ilipo nyumba yao.

Aidha John amesema mpaka sasa hawafahamu sababu ya mama yao kuuliwa.

Amesema mama yao alikuwa akiishi kwa miaka mingi katika mtaa huo na alikuwa akiishi na dada wa kazi huku akihudumiwa kwa karibu na kaka yake mkubwa ambaye hakumtaja jina.

“Hili tukio limetokea jana usiku. Kaka aliporudi nyumbani kutoka kwenye majukumu yake alimtafuta mama na alijaribu kupigia simu lakini haikupokelewa.

“Wakati akiendelea kumtafuta ndipo waliipata simu ikiwa na damu nyingi, kiatu kimoja mwili ukiwa umeburuzwa nje ya bom,” amesema mtoto wa marehemu.

Tatu Juma ambaye ni jirani wa marehemu, amesema kuwa bibi huyo alikuwa mcheshi na alikuwa akiongea vizuri na watu.

Amesema siku ya tukio walipata taarifa kisha kufika nyumbani kwake ndipo walianza kumtafuta bila mafanikio hadi alipopatikana mwili wake ukiwa umefunikwa na mawe eneo la kwa masikini jirani na nyumbani kwake.

“Huyu Bibi Mzungu ni jirani yangu amehamia hapa kwa muda mrefu sana na alikuwa hana tatizo na mtu ni mcheshi na sijawahi kusikia amegombana na mtu hapa mtaani lakini hili tukio lililotokea limenisikitisha sana,”  amesema jirani wa marehemu.

Kwa upande wake mjumbe wa Serikali ya Mtaa Bongola Shabani Juma alisema tukio hilo limetia doa mtaa huo na ameliomba Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwapata waliohusika.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim kuzungumzia suala hilo, hazikufanikiwa baada ya mwandishi wa habari hizi kumsubiri muda mrefu ofisini kwake bila mafanikio.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live