Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bibi adaiwa kuwachoma moto watoto wa mke aliyemuoa kimila

Bibi Awachoma Moto Bibi adaiwa kuwachoma moto watoto wa mke aliyemuoa kimila

Wed, 1 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Watoto watatu wa familia moja wamelazwa katika Hospitali ya Shirati wilayani Rorya wakiwa na majeraha ya kuchomwa moto na kupigwa sehemu mbalimbali ya miili yao na mtu anayedaiwa kuwa ni bibi yao.

Mbali na majeraha hayo watoto hao pia wana alama zinazoashiria kuwa walikuwa wakifungwa kamba miguuni na bibi huyo ambaye anadaiwa alimuoa mama yao kwa taratibu za kimila zijulikanazo kama Nyumba Ntobhu.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Shirati, Dk Chirangi Bwire amesema kuwa waliwapokea watoto hao jana Januari 31, 2023 saa 8 mchana huku mmoja akiwa na hali mbaya.

"Watoto wana majeraha sehemu mbambali za miili yao majeraha mengine yalikuwa yanatoa usaha na mengine yanaonekana ni ya siku nyingi kwa ufupi ni kwamba hawa watoto walikuwa wanafanyiwa ukatili kwa muda mrefu," amesema.

Amesema kuwa ingawa watoto hao wamepata tiba na hali zao kuanza kuimarika lakini upo uwezekano wa kuwa majeraha waliyo nayo yakawa yameingia hadi kwenye mifupa hivyo wapo kwenye mchakato wa kuwafanyia uchunguzi zaidi ili kujua madhara yapo kwa kiwango gani.

"Upo uwezekano wa hawa watoto kuwa wamepata majeraha hadi kwenye mifupa kwa hiyo tunataka kufanya uchunguzi zaidi ikiwepo kuwapiga x ray tuone madhara ni kwa kiwango gani maana hadi sasa baadhi ya majeraha bado yanatoa usaha na wana dalili za kuwa na bakteria wengi kwenye damu," amesema.

Dk. Bwire ameongeza kuwa watoto hao pia wamebainika kuwa na utapiamlo mkali hivyo idara ya lishe hospitalini hapo tayari imeanza kufanyia kazi changamoto hiyo huku wakiiomba Serikali kutia msaada wa ushauri wa kisaikolojia kwa watoto hao ambao wanaonekana kuishi kwenye mateso kwa muda mrefu.

Akizungumza baada ya kutembelea watoto hao, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amemtaja mtuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni Eliza Odira (68) mkazi wa Mtaa wa Obwere Shirati.

Amesema kuwa bibi huyo anayedaiwa kumuoa mwanamke mwezie anadaiwa kuwafanyia watoto hao vitendo vya kikatili kwa muda mrefu na kwamba baada ya taarifa hizo kupatikana polisi walifika nyumbani kwake na kuwakuta watoto hao wakiwa katika hali mbaya na kulazimika kuwawahisha hospitalini huku bibi huyo akipelekwa kituo cha polisi kwa mahojiano.

"Jambo la ajabu ni kwamba huyu bibi baada ya kuona hana uwezo wa kuzaa alimtafuta binti mdogo na kumuolea mume wake sasa yule binti yeye kazi yake ni kuzaa na huyu bibi anawachukua watoto kwa madai kuwa anawalea lakini matokeo yake ndiyo kama haya watoto wanafanyiwa ukatili na hata shule hawajaandikishwa," amesema.

Chikoka ameongeza kuwa watoto hao wamekuwa wakikumbana na vitendo vya ukatili kutoka kwa bibi huyo ambaye mbali na kuwachapa viboko na kuwafunga kamba pia amekuwa na tabia ya kuwachoma na moto sehemu mbalimbali za miili yao.

"Bibi amechimba shimo mle ndani kwahiyo akitaka kuwaadhibu anawasha moto na kuanza kuwachoma pamoja na vitendo vingine vya kikatili kubainika jana na kumkamata," amesema.

Amesema watoto hao ambao majina yao yanahifadhiwa wana umri wa miaka 6 hadi 2 na kwamba vitendo vya ukatili havikubaliki wilayani humo huku mama yao hao watoto Emily Bernard (25) amesema kuwa mara ya mwisho kuwaona watoto hao ilikuwa mwezi Septemba mwaka jana.

"Mimi naishi Kirogo na mwanaume sasa huyu bibi yeye ndiye hajaishi hapa Shirati na watoto sababu yeye ndiye aliyenitolea mahari ya ng'ombe wawili kwa ajili ya kuolewa na mume wake kwa sababu yeye alikuwa hazai kwa hiyo mimi na mume wangu tunaishi pamoja," amesema.

Chanzo: Mwananchi