Tafiti mbalimbali kuhusu haki za watoto na wazee zinaonesha vijana wengi wamewatwika mzigo mama na baba zao ambao kwa sasa ni wazee kuwalelea watoto wao.
Utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), wilayani Kisarawe mkoani Pwani mwaka 2017, ulibaini watoto wengi wanalelewa na babu au bibi zao vijijini ambao ni wazee huku watoto wa aina hii wakitajwa kuwa kwenye hatari ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia.
Askofu William Mwamalanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu ya Umoja wa Madhehebu ya Dini, anasema chombo chao pia kimebaini uwepo wa tatizo hili hasa katika mikoa ya Dodoma, Njombe, Kilimanjaro, Pwani na Tanga.
Tafiti hizo zinajidhihirisha hata kwa Agatha Litunu (69) na mumewe Ally Abdallah (70) wakazi wa Kinondoni Shamba ambao ni miongoni mwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini ulio chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf). Wazee hao wanawalea wajukuu wanane walioachiwa na watoto wao.
Agatha anasema yeye na mumewe ni wazee wanaohitaji kulelewa, lakini wanakabiliwa na changamoto ya kulea wajukuu wanane ambao wametelekezwa na wazazi huku baadhi wazazi wao wakiwa wamefariki dunia.
“Kuna wengine wanabahati kwa kuzaa, lakini mimi sina. Watoto wangu wengi ni wa kuzaa tu na kuniletea watoto. Hawaolewi wala kuoa waliobahatika ni wawili tu kati ya watoto wangu wanane. Mimi na mume wangu ndiyo tumebeba jukumu la kulea watoto wao,” anasema.
“Kila siku mume wangu anaamka saa 11 alfajiri kwenda Ilala kununua mahitaji ya gengeni na kuuza. Mimi nahakikisha wajukuu wangu asubuhi wanakunywa chai na kwenda shule.
“Kwa siku tunatumia Sh24,300 kuhudumia familia kwa maaana ya chakula cha asubuhi, mchana, jioni na fedha za masomo ya ziada. Kila mmoja nampatia Sh1,000. Gharama zote hizi zinategemea gege ambalo nimelifungua baada ya kupata fedha kutoka Tasaf,” anasema.
Agatha na mumewe waliamua kuchukua jukumu la kulea wajukuu baada ya watoto wao wanne kufariki kwa ugonjwa wa ukimwi na mwingine kukimbilia Afrika Kusini miaka 20 iliyopita na kumwachia mtoto mdogo ambaye mwaka huu amehitimu kidato cha nne.
“Tumezaa watoto wanane, kati yao wanne walikufa na mmoja alikimbilia Afrika Kusini, sijui kama ni mzima au amekufa, mtoto wangu mwingine huyo ni mlevi ni mtu wa kutangatanga na yeye anatutegemea sisi. Wawili wapo na maisha yao lakini hawana uwezo wa kujihudumia,” anasema.
Kwa upande wake Abdallah (mume wa Agatha) anasema licha ya uzee walionao wamejikuta wakibeba jukumu zito la kulea wajukuu hao ambao wakati mwingine wanashindwa kuwalea vyema kimaadili kutokana na uzee na kipato duni.
“Tulijiunga na Tasaf miaka mitatu iliyopita walau inatusaidia, kwa mara ya kwanza tulipewa Sh68,000 ambayo tulianzisha biashara ya kukaanga mihogo, baada ya hapo tukaamua kufungua genge kwa mtaji wa Sh50,000 ambalo sasa linamtaji wa Sh200,000,” anasema.
Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kinondoni Shamba, Petro Mayanja anakiri kuwepo tabia za wazazi kuwatelekeza watoto wao na kuwapa mzigo wazee na mara nyingi watoto wanaolelewa na wazee wamekuwa na matatizo mitaani.
Anasema anaitambua familia ya Agatha na kudai kuwa wazee hao wanalea wajukuu zao na taarifa alizonazo baadhi ya wajukuu ni yatima.
Kaimu mratibu wa Tasaf Wilaya ya Kinadoni, Gladness Macha alisema moja ya changamoto wanayokutana nayo katika kutekeleza mradi huo ni wazazi kuwatelekeza watoto kwa bibi na babu zao.