Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biashara ya ‘dada poa’ yakithiri Singida

MAKAHABA Biashara ya ‘dada poa’ yakithiri Singida

Wed, 27 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Arusha uliopo Kata ya Minga, wamelalamikia kurejea biashara ya kuuza miili, maarufu kama ‘dada poa’ inayofanywa katika vichochoro vya mitaa hiyo usiku.

Wakazi wa eneo hilo mkoani hapa, walisema vichochoro hivyo vipo jirani na baa maarufu ya Kirima ambako biashara ya ‘dadapoa’ hufanyika nje nje kuanzia jioni.

Walidai ‘dadapoa’ wanasababisha watoto wao wa kike na wa kiume kujiingiza katika shughuli hio.

Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa azungumzie kero hiyo, ambaye alisema wanaendeleza doria za mara kwa mara zikiwa na lengo la kuimarisha hali ya usalama kwa wananchi wote.

Alisema katika doria iliyofanyika hivi karibuni wamewakamata baadhi ya wadada wanaojishughulisha na biashara hiyo aliyoiita kuwa ni haramu.

“Tumeendeleza doria za kila mara, hivi karibuni tumefanya doria na tumewakamata hao wanaojishughulisha na hiyo biashara,” alisema Mutabihirwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Arusha, Saidi Shabani alisema katika eneo hilo upande mmoja husimama wadada na mwingine watoto wa kiume wenye umri kati ya miaka 15 hadi 20 wanaosoma kidato cha tatu hadi cha nne.

Alisema juhudi walizozifanya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi za kufanya doria na kuwakamata ziligonga mwamba kutokana na kurejea kwa biashara hiyo ndani ya miezi mitatu.

Mkazi wa mtaa huo, Mwanaimu Omary alisema wadada hao huwakaba vijana hasa wa kiume wanaopita maeneo hayo usiku wakiwa wanarejea nyumbani huku wakifanya shughuli zao hizo kwenye nyumba za kulala wageni katika mtaa huo na wengine hufanya maeneo ya wazi.

Shekh Ally Salum ambaye ni Imam wa Msikiti wa Kati Singida, alisema dini yao inakemea vikali vitendo hivyo kwa sababu vinachangia athari kubwa ya kimaadili kwa jamii.

Askofu wa Kanisa la Penyekoste, Dk Paul Samweli alisema wanashindwa kuchukua hatua za moja kwa moja bali wanaishia kwenye kuwahubiria watu kuacha vitendo hivyo kwa kuwa ni chukizo mbele ya Mungu na kwa wanadamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live